PASAKA YA KATIBA
“Sote tuwe na umoja” (Yn. 17:21)
Nimesoma kwa kina Tamko la Maaskofu Thelathini na Wawili wa Kanisa
Katoliki Tanzania. Pia nimepitia taarifa za magazeti yote nchini
yaliyoandika kuhusu salamu za Sikukuu ya Pasaka kwa Wakristo nchini na
Watanzania kwa ujumla. Mwenendo wa Bunge la Katiba umeshamiri katika
matamko ya Viongozi wetu wa Dini katika mahubiri yao ya Sikukuu ya
Pasaka.
Napenda kuwashukuru kwa Maaskofu wetu kwa Hekima na Busara ya hali ya
juu katika matamko yao na wito wa kutaka mchakato wa Katiba uendelee
kwa kuheshimu maoni ya Wananchi na kuboresha inapobidi ili kupata Katiba
bora. Kama nilivyopata kusema hapo awali, Katiba ni Mwafaka wa Taifa
kwa hiyo ni lazima kila mmoja wetu awe na moyo wa maridhiano. Makundi
makubwa ya Kisiasa nchini yanapasa kuunga mkono kwa vitendo Tamko hili
la Maaskofu pamoja na rai mbali mbali ambazo Viongozi wetu wa kiroho
wametoa wakati huu wa Sikukuu ya Pasaka.
Maaskofu wanatukumbusha Nanukuu; “Tulichukua hatua kubwa kuunganisha
nchi mbili huru, Tanganyika na Zanzibar, na kuifanya kuwa nchi moja ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa kielelezo kwa Bara la Afrika cha
kujenga umoja”. Wanaendelea “Pamoja na mafanikio hayo makubwa,
zimejitokeza dosari kadhaa katika umoja zilizofanya umoja wetu upoteze
baadhi ya sifa zake za awali. Kupungua kwa hisia za kujisikia watu wote
ni taifa moja, ni dosari iliyoanza kukua taratibu na sasa inaonekana
kuwa ndio ukweli. Baadhi ya Watanzania wanafikiri kuwa umoja unaofuta
tofauti haufai ila umoja unaosisitiza tofauti kama ulivyo umoja wa
kikanda (kama ilivyo SADC, ECOWAS, n.k) ndio unafaa! Wakati mataifa
mengine yanatamani umoja unaofanana na ule umoja wetu wa awali, baadhi
yetu tunatamani kurudi nyuma kwenye umoja wa mpito!”
Ni dhahiri viongozi wetu wa kiroho wanaumizwa na juhudi zinazoendelea
za kuuzongazonga Muungano na hata kuhoji uhalali wake kiasi cha baadhi
ya Watanzania kutaka tuwe Jumuiya ya Kiuchumi tu. Tunaonywa pia kuhusu
Muungano wenye Serikali ya Muungano ‘egemezi na tegemezi’ iwapo
hatutaboresha Rasimu ya Katiba. Vilevile viongozi wetu wa dini
wanasikitikia uwezekano wa Muungano kuvunjika. Hata hivyo wanaonyesha
kwamba Rasimu ya Katiba imeweka misingi mizuri ya kuendeleza Mshikamano
na Umoja wetu. Wanasema;
“Vigezo vyote muhimu kwa maisha ya mshikamano kitaifa vimeandikwa katika Rasimu ya Katiba Sura ya 1 hadi ya 5. Tukisha kukubaliana na yaliyomo katika sura hizo, muundo wowote wa Serikali unawezekana kwa kuzingatia kanuni za uwiano wa madaraka na wajibu wa mihimili mitatu ya Dola kwa mujibu wa Sura za 8 hadi 15”. Wanaendelea, “Chaguo la muundo wa Dola, sharti liongozwe na malengo na madhumuni ya umoja wetu wa kutaka tuishi kwa mshikamano wa dhati. Uchaguzi wa muuungano wa serikali moja, mbili au tatu sharti ufanywe kwa dhamiri safi iliyo na uelewa uliochambua matatizo yaliyopo ya Muungano na kuridhia mfumo utakaosuluhisha matatizo hayo pasipo mashaka yoyote”
Katika Salamu zake na Pasaka, Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi
ya Dar es Salaam Dkt. Valentino Mokiwa naye pamoja na kulaani vikali
mwenendo wa Bunge la Katiba ametaka pia Muundo Muungano ikibidi uwe na
Rais mmoja tu na wengine wawe wasaidizi wake. Hii inarutubisha hoja ya
kuboresha Rasimu ya Katiba ili kupata Katiba inayopendekezwa
itakayopelekwa kwa Wananchi na kuamuliwa kwa kura. Kwa maoni yangu, ni
vema Wajumbe wote wa Bunge la Katiba kuweka mawazo yao wazi badala ya
kung’ang’ania misimamo ya Vyama vyao vya siasa au Makundi yao. Wanaotaka
Serikali Mbili (S2) wawasikilize wanaotaka Serikali Tatu (S3) kama
zilivyo kwenye Rasimu na vilevile wanaotaka Tatu zilizoboreshwa (S3z)
nao pia wasikilizwe. Hatimaye tupate Katiba bora inayopendekezwa. Neno
Dhamira Safi ni neno la msingi na la kuzingatia sana katika mchakato
huu. Ni vema wenzetu wasiotaka Muungano wawe wazi badala ya kujificha
kwenye miundo.
Maaskofu wetu wanatusihi nanukuu, “Tunalisihi na kulishauri Bunge
Maalum la Katiba kuheshimu mawazo yaliyowasilishwa na kutumia busara
zilizopendekezwa za kujenga muundo wa Muungano utakaokidhi mahitaji ya
utangamano, mshikamano, amani, maadili, uhuru na uwajibikaji wa viongozi
na raia wa Tanzania”. Kwa upendo kabisa viongozi wa Dini wanatuombea, “Wakati
huu wa Pasaka, tuendelee kuliombea Bunge Maalumu la Katiba ili wajumbe
wawe wazingatifu wa matakwa na matarajio ya Watanzania yalivyoainishwa
katika Rasimu ya Pili ya Katiba na Tume ya mabadiliko ya Katiba kwa
kuheshimu maoni ya Watanzania na kuboresha maoni hayo kwa hekima na
busara ili kulinda mstakabali wa Taifa letu”.
Licha ya kuombewa na viongozi wetu hatuna budi sote kwa pamoja
kulaani na kukataa lugha za matusi na kibaguzi zilizogubika majadiliano
ya Bunge Maalumu la Katiba. Askofu Mkuu wa KKKT Dkt. Alex Malasusa
amekemea vitendo vya kibaguzi na kusisitiza umuhimu wa kusikilizana,
kuheshimiana na kuridhiana. Wakati Kardinali Pengo anasihi Wajumbe
waliotoka nje kurejea Bungeni ni vema basi viongozi wa dini zetu zote
kuu, Waislam na Wakristo, pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania wachukue wajibu wa kwanza, kuendelea kukemea vikali lugha za
kibaguzi, matusi na kejeli. Viongozi wa Bunge la Katiba wachukue jukumu
la kuwaadhibu Wajumbe wanaotoa lugha za namna hii wakati wa mijadala na
viongozi wa vyama vya siasa waweke nidhamu kwa wanachama wao. Ninashauri
Viongozi wetu wa Dini kukaa pamoja na Viongozi wa makundi ya kisiasa
katika Bunge Maalumu ili kupata maridhiano, kujenga kuaminiana na
kusonga mbele. Ni vema mkutano huu wa maridhiano chini ya Viongozi wakuu
wa Dini zetu ufanyike kabla ya Sikukuu ya Muungano. Nawasihi viongozi
wetu wa kisiasa kukubali maridhiano kupitia kwa viongozi wa dini zetu
kwani maridhiano yanajenga Mwafaka na Katiba ni Mwafaka Mkuu wa Kitaifa.
Maaskofu wamenena. Tusikie. Pasaka iwe ya Maridhiano katika kuandika
Katiba. Mateso aliyopata Bwana Yesu na kisha kufufuka kwake iwe rejea
yetu na kusameheana pale tulipokoseana na kuweka misingi ya
kuheshimiana, kusikilizana na kuridhiana.
Zitto Kabwe, MB
Dar-es-Salaam,
Jumatatu 21/04/2014
No comments:
Post a Comment