Friday, June 27, 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU UCHAGUZI MKUU SIMBA, UWANJA ULIOPO BUNJU




KAMATI ya Uchaguzi ya Simba SC inapenda kuwaalika wanachama wote wa Simba katika Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Klabu uliopangwa kufanyika Keshokutwa Jumapili, Juni 29 mwaka huu, katika Ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Shughuli za uhakiki wa wanachama zitaanza saa moja kamili asubuhi na Mkutano umepangwa kuanza saa tatu kamili asubuhi na wanachama na wagombea wote wanaombwa kuwa wamekaa katika viti vyao kufikia muda huo.

Katika uchaguzi huo, jumla ya wagombea 27 wanatarajiwa kushiriki na Kamati ya Uchaguzi imeazimia kwamba suala la muda litazingatiwa sana safari hii kutokana na ukweli wa kuwepo kwa wagombea wengi.
 
Ni matumaini ya Kamati ya Uchaguzi ya Simba SC kwamba wanachama watazingatia muda wa kufika ili kurahisisha shughuli za kamati.
Kamati inatangaza pia kwamba katika uchaguzi huo, ulinzi utakuwa wa kiwango cha juu; ingawa ina matumaini kwamba wanachama wote watakuwa watulivu ili kulinda jina, heshima na hadhi ya Simba SC.
 
Benki ya Posta
Wanachama wanatangaziwa kwamba kwenye uchaguzi kutakuwa pia na huduma ya kutoa kadi kwa washabiki wa Simba wanaotaka kuingia katika mfumo mpya wa Benki ya Posta. Simba na Benki ya Posta zimeingia katika makubaliano ya kutengeneza kadi hizo ambazo kwa utaratibu utakaotangazwa katika siku zijazo, ndiyo zitatumika kwa wanachama wote.

Uwanja Bunju
Uongozi wa Simba unawakaribisha wapenzi na wanachama wake kesho Jumamosi katika Uwanja wa Klabu uliopo katika eneo la Bunju jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya ujenzi wa uwanja wa mazoezi wa klabu. Ujenzi huo ulioanza miezi miwili iliyopita, unakaribia kukamilika na utakuwa uwanja wa kwanza rasmi wa mazoezi wa klabu katika historia yake.
 

Vyombo vya habari navyo vinaalikwa katika tukio hilo litakaloanza saa tano kamili asubuhi.
 

Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Katibu Mkuu
Simba SC


No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...