Maoni kuhusu Muungano v Shirikisho
Zitto Kabwe, Mjumbe, BMK
Iwapo Tanzania ni Shirikisho (Federation) au ni Muungano (Union) ni
jambo ambalo limekuwa likuzua utata kwa miaka mingi. Hivi sasa katika
vikao vya Kamati za Bunge maalumu la Katiba jambo hili limezua mjadala
mkubwa ambapo baadhi ya Wajumbe wanapendekeza kuwa neno Shirikisho
litoke kwenye sura ya kwanza ya Rasimu ya Katiba na wengine
wakipendekeza libakie au hata kuweka wazi kabisa kuwa Tanzania ni
Jamhuri ya Shirikisho la Tanganyika na Zanzibar. Maoni haya yanatokana
na misimamo ya wajumbe kuhusu muundo wa Muundo wa Muungano kwa maana ya
idadi ya Serikali. Ni vema dhana hizi kueleweka vizuri ili watumiaji
waweze kuzitumia kwa usahihi. Kwa ufupi tutazame maana ya kila dhana na
mifano mbalimbali duniani. Tutatazama dhana tatu kuu – Muungano (Union),
Shirikisho (Federation) na Jumuiya (Confederation/Community).
Muungano (Union)
Katika aina hii ya Nchi kuungana huundwa Taifa moja, Dola moja ndani
ya Nchi moja. Katika muundo huu Serikali za Washirika wa Muungano
huachia sehemu kubwa ya madaraka yao kwa Serikali ya Muungano. Mara
nyingi muundo huu hupelekea kuwapo kwa Serikali moja yenye nguvu ya
Muungano na kama Washirika wanabakia na Serikali zao, basi hubakia na
mambo machache sana. Faida ya Muundo huu ni kwenye uimara wake na sio
rahisi kuvunjika. Hasara za muundo huu ni athari ya moja ya nchi, hasa
kama ni ndogo, kumezwa na Mshirika mkubwa. Hapa Afrika Nchi ya Afrika ya
Kusini (Republic of South Africa) inafuata muundo huu wa Muugano ambapo
Serikali ya Muungano ina nguvu na mamlaka mengi kuliko Serikali za
Majimbo yanayounda Jamhuri ya Afrika ya Kusini. Huko Asia mfano mzuri ni
Nchi ya India ambapo japo muundo wake unatoa nguvu kubwa kwa Majimbo
kujitawala, Serikali ya Muungano (Union Government) ina nguvu kubwa
zinazoondoa sifa ya kuitwa Shirikisho. Sio lazima ‘Union’ kuwa na
Serikali moja (Unitary State) isipokuwa mazingira ya nchi husika ndio
yanaweza kuamua. Mfano mzuri hapa ni ule wa Afrika ya Kusini ambayo ni
‘unitary state’ yenye Serikali 10, tisa za Majimbo na Moja ya Muungano.
Shirikisho (Federation)
Katika muundo huu Serikali za Washirika hukasimu sehemu ndogo ya
madaraka yake kwa Serikali ya Muungano. Mambo ya kidola (sovereign
functions) hufanywa na Serikali ya Shirikisho na Serikali za Washirika
kubakia na mambo yake yenyewe. Kwa mujibu wa Sheria za kimataifa nchi
yenye mfumo wa Shirikisho kuwa ni nchi moja katika sura ya kimataifa
ingawa inawezaonekana ni nchi zaidi ya moja ndani ya Shirikisho husika.
Faida kubwa ya muundo huu ni kuondoa hofu ya mkubwa kummeza mdogo na ule
uhuru wa kujiamulia mambo mengi. Hasara ya muundo huu ni kujengwa kwa
utaifa au hisia za utaifa za Washirika ambazo hatimaye hupelekea
Shirikisho kuvunjika. Hapa Afrika mfano mzuri wa Shirikisho ni nchi ya
Ethiopia ambapo Majimbo yake yanao uwezo hata wa kujitoa katika
Shirikisho kikatiba. Eritrea ilitumia fursa hii na kujitoa kuwa sehemu
ya Ethiopia mara baada ya mapinduzi yaliyomtoa Mengistu Haile Mariam.
Ujerumani pia ni Shirikisho (Federal Republic of Germany au kwa
kijerumani BundesRepublik Deutschland)
Jumuiya (Confederation/Community)
Katika muundo huu kila Mshirika anakuwa na uhuru wa mambo yake yote
isipokuwa tu kunakuwa na mambo ya uratibu wa pamoja. Aina hii ya Muundo
ndio unapaswa kwa kinachoitwa Muungano wa Mkataba. Faida kubwa ya muundo
huu ni kwamba hakuna kubanana na pale kunapotokea hofu Mshirika
hujitoa. Hasara yake imo kwenye faida yake.Mfano mzuri ni Switzerland na
Jumuiya ya Ulaya. Hata Jumuiya ya Afrika Mashariki pia inaitwa kuitwa
ni Muungano wa Mkataba.
Muundo gani Tanzania?
Tanzania kuwa Shirikisho au Muungano ni mjadala ambao utaendelea
kuwapo licha ya kuamua kuchagua muundo mmoja wapo. Wakati wa kuandika
Katiba ya India mwaka 1947 ubishani huu ulikuwa mkubwa sana pia. Katiba
ya India imegawanya mamlaka katika sehemu tatu – Mambo ya Muungano,
Mambo ya Washirika na Mambo ya pamoja (concurrent). Wajumbe wa Bunge la
Katiba la India wanaotaka Shirikisho walipinga muundo huo na kukataa
‘Washirika kuwa ombaomba kwa Serikali ya Muungano’. Hata hivyo ubishi
huo ulimalizwa na Mwanasheria mahiri wa India bwana B M Ambedkar kwa
kusema ‘tunataka Serikali imara ya Muungano na yenye nguvu iwezekanvyo’
na alifunga mjadala kwa kusema ‘Muungano wa Washirika unatakiwa zaidi
kuliko Shirikisho la Washirika’. Hivi ndivyo ilivyo India ambapo pamoja
kwamba ni Shirikisho lakini ni ‘Unitary’. Vile vile Jamhuri ya Afrika ya
Kusini ina muundo sawa sawa na nchi ya Jamhuri ya Shirikisho la
Ujerumani lakini wakati Ujerumani ni Shirikisho, Afrika Kusini ni
Muungano (Unitary).
Watanzania hatupaswi kuiga isipokuwa kujifunza kwa nchi nyingine.
Hivyo muundo gani unafaa ni uamuzi wetu wenyewe. Hata hivyo uamuzi huo
ni lazima ujibu vigezo fulani fulani. Vigezo vikubwa ni viwili; Je,
Muundo tunaoutaka utajibu kero (malalamiko) za Muungano wa sasa? Je,
Muundo tunaoutaka utajibu hofu za Muungano kuvunjika. Muundo utakaojibu
hofu hizo ndio utakaotufaa. Tanzania inaweza kuwa na Muundo wa Muungano
wenye Serikali tatu ama Muundo wa Shirikisho wenye Serikali mbili, ama
kinyume chake. Idadi ya Serikali haina uhusiano wowote na ama tunaitwa
Shirikisho au Muungano. Mifano miwili hapo juu ituongoze, India ni
Muungano unaitwa Shirikisho na Afrika Kusini ni Shirikisho linaloitwa
Muungano. Tanzania inaweza kuwa vyovyote vile ili mradi tu kunakuwa na
Mamlaka ya kutosha katika masuala ya Muungano ili kuiweka Nchi pamoja na
kuwa na Taifa imara mbele ya mataifa ya ulimwengu.
Muungano wa Serikali 3 na sio Shirikisho la Serikali 3 ndio
mapendekezo yangu. Muungano (Union) wa Washirika ni bora, imara na
endelevu zaidi kwa mazingira ya Afrika kuliko Shirikisho (Federation) la
Washirika.
Mapendekezo yangu mahususi yaliyowasilishwa kwenye kamati namba 12 ni kama ilivyo hapa chini.
SURA YA KWANZA
SEHEMU YA KWANZA
1(1) Irekebishwe na kuandikwa upya na isomeke
Tanzania ni Nchi Moja na ni Jamhuri ya Muungano yenye mamlaka kamili
ambayo imetokana na Muungano wa Nchi za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri
ya Watu wa Zanzibar ambazo kabla ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ya
Mwaka 1964, zilikuwa nchi huru.
1(2) neno Shirikisho lifutwe na kuongeza maneno ….Nchi ya…. baada ya neno ‘ni’ na kabla ya neno ‘kidemokrasia’
Ongeza ibara ya mpya ya 3 itakayosomeka
3(1) Shughuli zote za Mamlaka ya Nchi katika Jamhuri ya Muungano
zitatekelezwa na kudhibitiwa na vyombo vitatu vyenye mamlaka ya
Utendaji, vyombo vitatu vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki, na pia
vyombo vitatu vyenye madaraka ya kutunga sheria na kusimamia
utekelezaji wa shughuli za umma
3(2) Vyombo vyenye Mamlaka ya Utendaji vitakuwa ni Serikali ya
Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika;
vyombo vyenye Mamlaka ya kutekeleza utoaji haki vitakuwa ni mahakama ya
Juu ya Jamhuri ya Muungano, Mahakama ya Tanganyika na Mahakama ya
Zanzibar na vyombo vyenye Mamlaka ya ya kutunga sheria na kusimamia
utekelezaji wa shughuli za umma vitakuwa ni Bunge la Jamhuri ya
Muungano, Baraza la Wawakilishi la Tanganyika na Baraza la Wawakilishi
la Zanzibar.
3(3) Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za umma katika Jamhuri
ya Muungano, na kwa ajili ya mgawanyo wa madaraka juu ya shughuli hizo
baina ya vyombo vilivyotajwa katika ibara hii, kutakuwa na mambo ya
Muungano kama yalivyoorodheshwa katika Nyongeza ya Kwanza ya Katiba hii,
kutakuwa na mambo ya uratibu wa pamoja na kutakuwa na mambo yasiyo ya
Muungano ambayo ni mambo mengine yote yasiyo mambo ya Muungano na yasiyo
ya uratibu wa pamoja.
3(4) Kila chombo kilichotajwa katika ibara hii kitaundwa na
kutekeleza majukumu yake na Katiba za Serikali za Washirika na kwa
kufuata masharti ya katiba hii.
3(5) Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Serikali ya Jamhuri
ya Muungano au Serikali ya Tanganyika au Serikali ya Zanzibar Bunge
laweza kuigawa Jamhuri ya Muungano katika Mikoa kwa mujibu wa Sheria
iliyotungwa na Bunge Isipokuwa kwamba Bunge litapata kwanza Azimio la
Baraza la Wawakilishi la Tanganyika kwa mikoa ya Tanganyika au Baraza la
Wawakilishi Zanzibar kwa mikoa ya Zanzibar.
SABABU ZA MAREKEBISHO YANAYOPENDEKEZWA.
Rasimu ya Katiba imetangaza tu kuwa ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
(JMT) ni Nchi’ na kuacha ‘ambiguity’ ya kwamba Tanzania ni nchi ngapi.
Katiba ya sasa imetamka bayana kuwa ‘Tanzania ni Nchi Moja’. Rasimu
pia imetamka kwamba JMT inatokana na ‘muungano wa nchi mbili’. Hivyo
basi ni vema kuweka wazi kabisa kuwa Nchi hizi mbili zimeunda nchi moja.
Hii itaepusha migongano ya siku za usoni kuhusu tafsiri ya Katiba na
Mamlaka za Nchi. Ifahamike wazi kuwa idadi ya Serikali haina uhusiano na
uundaji wa nchi moja.
Rasimu imetangaza kuwa Tanzania ni Shirikisho ingawa bado imetamka
‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (United Republic of Tanzania). Dhana za
‘Union’ na ‘Federation’ ni dhana mbili tofauti katika miungano.
Idadi ya Serikali haina mahusiano ya moja kwa moja na aina ya
Muungano kama ni ‘Union’ au ni ‘Shirikisho’. Kwa mazingira ya Nchi za
Kiafrika ni salama zaidi kuwa na ‘Union’ kuliko Shirikisho. Kwa kutumia
maneno ya Mwanasheria gwiji na mwandishi wa Katiba ya India Bwana B M
Ambedkar, “Muungano wa Washirika unatakiwa zaidi kuliko Shirikisho la
Washirika”. Ni vema kuwa na Muungano wenye Serikali ya Muungano yenye
nguvu iwezekanavyo ili kuhimili vishindo na changamoto dhidi ya Nchi
yetu na umoja wetu bila kuathiri uhuru wa Serikali za Washirika
kuendesha mambo yao wenyewe bila bugudha.
Rasimu imeweka sura ya Kwanza bila kutaja vyombo vya Jamhuri ya
Muungano. Ni vema ili kuondoa ‘ambiguity’ vyombo vya Jamhuri ya Muungano
kutajwa kinagaubaga katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano katika sura ya
‘uundwaji wa nchi’. Mapendekezo ya ibara mpya za sehemu ya kwanza ya
sura ya kwanza yanazingatia tahadhari hiyo. Katika kutaja vyombo
mapendekezo haya yanaonyesha dhahiri kuwa ugawaji wa Nchi katika Mikoa
inakuwa ni mamlaka ya Bunge. Serikali za Washirika zaweza kuwa na
mamlaka ya Serikali za Mitaa. Mikoa inapaswa kuwa mamlaka ya Bunge la
Muungano kwa sababu yaweza pia kutumika katika kupata Wabunge wa
Muungano lakini pia itasaidia kuondoa tabia ya kugawa mikoa hovyohovyo.
Kimsingi ilipaswa Mikoa yote ya Nchi itajwe ndani ya Katiba kuongezeka
au kupunguka kwake kutokane na maamuzi maalumu ya Bunge hata ikibidi iwe
kwa theluthi mbili.
SURA YA SITA
Ibara ya 60(1) maneno shirikisho yafutwe na kubaki uwepo wa Serikali 3.
60(3) isomeke
Muundo, madaraka na mambo mengine ya kiutendaji yahusuyo Serikali ya
Tanganyika, na Serikali ya Zanzibar yataanishwa katika Katiba za
Washirika na kwa kuzingatia masharti ya Katiba hii.
Ibara ya 63 iitwe 63(1)
Iongezwe 63(2)
Kwa ajili ya uratibu bora wa shughuli za Mamlaka za Nchi na kwa ajili
ya kuhakikisha ufanisi na weledi katika uendeshaji bora wa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mgawanyo wa madaraka, Serikali ya
Jamhuri ya Muungano itakuwa na mamlaka ya uratibu juu ya mambo ya
uratibu kama yalivyoorodheshwa katka nyongeza ya pili ya Katiba hii.
64(1) maneno nchi washirika yaondoke na kubakia neno Washirika au Washirika wa Muungano.
64(5) isomeke
Serikali za Washirika zitakuwa na hadhi na haki sawa ndani ya Jamhuri
ya Muungano na zitatekeleza majukumu yao kwa mambo yote yasiyo ya
Muungano katika mamlaka za Serikali za Washirika kwa mujibu wa masharti
yatakayowekwa na Katiba za Serikali za Washirika kwa kuzingatia masharti
ya Katiba hii.
65 maeneo yote yenye maneno Nchi Washirika yafutwe na kuandikwa Washirika wa Muungano
67 ifutwe yote
69 maneno Nchi yafutwe ….katiba za Washirika…….
69 (2) maneno Viongozi wakuu yafutwe na kuandikwa ‘ Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na Wakuu wa Serikali za Washirika watakuwa ni
Viongozi Wakuu wa Nchi’
69(3) isomeke
Viongozi wanaohusika na masharti ya ibara hii ni
(a) Rais wa Jamhuri ya Muungano
(b) Mkuu wa Serikali ya Tanganyika ambaye pia atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
(c) Mkuu wa Serikali ya Zanzibar ambaye pia atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Ongeza ibara ya 70
(1) Mkuu wa Nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ataitwa
Rais atapatikana kwa kuchaguliwa kwa kura na wananchi wote wa Jamhuri ya
Muungano kwa Mujibu wa masharti ya Katiba hii. Rais atakuwa pia Mkuu wa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
(2) Wakuu wa Serikali za Washirika watapatikana kutoka kwenye
Mabaraza ya Wawakilishi ya Washirika kutoka Chama cha siasa chenye
wawakilishi wengi kwa mujibu wa masharti yatakayowekwa na Katiba za
Washirika na kwa kuzingatia masharti ya Katiba hii.
SABABU ZA MAPENDEKEZO
Lengo ni kuhakikisha kuwa Jamhuri ya Muungano inabakia ni nchi moja
yenye serikali 3 zenye mamlaka na madaraka yake yaliyofafanuliwa na
katiba. Kwa kuwa tunaamua kuwa na Nchi moja basi Serikali zinazoundwa
zitakuwa ni Serikali Washirika na sio nchi Washirika tena kama rasimu
inavyoita. Kuweka wazi kuwa ni kiongozi mmoja tu wa Serikali ndio
atachaguiwa na wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano naye ni Rais – Mkuu
wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Ulinzi na usalama.
Majina ya Wakuu wa Serikali za Washrika yatatolewa na kwa mujibu wa
Katiba zao na hivyo hakuna sababu kwa Katiba ya Muungano kuunda majina
isipokuwa tu Wakuu wa Serikali za Washirika watakuwa ni Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano kwa kuzingatia kuwa iwapo Rais wa Muungano
anatoka upande mmoja wa Muungano, makamu wa kwanza atatoka upande wa
pili wa Muungano. Makamu wa Rais wanaweza kukaimu Urais kwa masharti
maalumu yatakayowekwa na Katiba.
Mapato na mgawanyo wa Mapato ya Muungano katika Serikali Tatu
Dola inapasa kuwa na rasilimali za kutosha na ziada inaweza kugawa
kwa Washirika na Mikoa katika wajibu wa kuhakikisha maendeleo yanawiana.
Dola pia inaweza kuwa na miradi ya Muungano. Kuna haja ya kuangalia kwa
umakini mkubwa suala hili la mapato ya Serikali ya muungano kama kweli
kuna nia ya dhati ya kuendelea kuwa na Muungano. Mapendekezo yangu ni
kama ifuatavyo;
Mapato ya Muungano
1. Ushuru wa Forodha
2. Mrahaba wa uvunaji wa Rasilimali ambapo 25% itabaki kwenye mkoa
wenye rasilimali na 75% itatumika na Serikali ya Muungano kugawa kwenye
mikoa kwa mujibu wa ‘formulae’ itakayokubaliwa kwa kuzingatia idadi ya
watu, kiwango cha umasikini na ukubwa wa kijiografia.
3. Ushuru wa Bidhaa na huduma ambapo 60% itagawiwa kwa nchi Washirika kwa ajili ya miradi maalumu ya muungano.
4. Mapato kutoka kwenye kampuni za kibiashara za Serikali ya Muungano na gawio la Benki Kuu ya Tanzania.
Mapato ya Serikali za Washirika
1. Kodi ya Mapato ya watu binafsi na Makampuni 2. Kodi ya Ongezeko la
Thamani au kodi kama hiyo 3. Tozo mbalimbali zitakazotungwa kwa mujibu
wa sheria 4. Mapato yasiyo ya kikodi kutoka idara na Wizara za Serikali.
Mapato ya Mikoa
1. 25% ya Mrahaba kutokana na uvunaji wa Rasilimali/maliasili
inayopatikana katika mkoa husika 2. 10% ya makusanyo ya kodi ya mapato
ya watu binafsi na makampuni kutoka katika mkoa husika 3. Mgawo kutoka
Serikali ya Muungano 4. Mgawo kutoka Serikali ya Washirika 5. Tozo
mbalimbali zitakazoanzishwa kwa mujibu wa sheria ndogo ndogo
zitakazopitishwa na Mabaraza ya Mikoa
Dodoma,
Aprili 2014
No comments:
Post a Comment