Mshambuliaji wa Lille ya
Ufaransa , Mkenya Divorc Origi ambaye ni mzaliwa wa Ubelgiji ni miongoni
mwa wachezaji wa timu ya taifa ambayo imeondoka Jumanne kuelekea Brazil
kwa mashindano ya kombe la dunia kuanzia Alhamisi wiki hii.
Origi, mwanae Mike Okoth, mchezaji wa zamani wa
timu ya taifa ya Kenya Harambee Stars atakua mchezaji wa kwanza wa
Afrika Mashariki kuiwakilisha Ubelgiji, na yuko pamoja na wachezaji
nyota kama vile Vincent Kompany wa Manchester City na Eden Hazard wa
Chelsea.
Watakabiliana na Algeria mechi yao
ya kwanza ya kundi H Juni tarehe 17 na siku tano baadae wanapepetana na
Urusi kisha Korea Kusini kwenye mechi za mchujo.
Akizungumza na BBC kwa njia ya simu akiwa
Ubelgiji Origi anasema:'' Algeria ni timu yenye wachezaji wazuri kwa
hivyo hatuwezi kuidharau. Tutacheza mchezo wetu wa kawaida lakini nina
matumaini makubwa tutashinda.’’ Anasema Urusi na Korea pia si timu
hafifu hasa Warusi. Lengo lake kubwa ni Ubelgiji kufuzu kwa raundi ya
pili kisha kutoka hapo anasema mambo yatakuwa sawa kabisa.
Kuhusu mbona ameamua kuiwakilisha Ubelgiji na
sio taifa la babake Kenya, Origi anasema alitilia maanani mambo mengi
kama vile usimamizi mzuri wa kandanda nchini humo, mizizi yake ya
kandanda iliyoko huko, marafiki, ushauri wa babake pamoja na Ubelgiji
kufuzu kwa kombe la dunia kwani haijulikani ni mwaka upi Kenya itafuzu
kwa kombe la dunia.
Tukiwa tunazungumzia hilo babake Origi, Mike
Okoth, naye anajitupa uwanjani kwa kusema:''Mimi nilimshauri aichezee
Ubelgiji na sio Kenya kwa sababu kusema kweli kama angechezea Harambee
Stars kuna mambo ambayo hangestahimili hasa usimamizi mbovu. Mimi
nilivumilia kwa saababu nimezaliwa Kenya lakini mwanangu hangeweza
kabisa. Na tena bado ni mchanga kwa hivyo ni vyema aiwakilishe Belgium.
Nakumbuka siku moja tukiwa na Harambee Stars tulilala kwenye jumba moja
ambalo bado lilikua linajengwa huko Afrika Magharibi.’’
Namuuliza Okoth kama kuna siku Harambee Stars
itafuzu kwa kombe la dunia? ''Itakua vigumu sana kwao kufuzu kwa kombe
la dunia kama usimamizi ni duni bado,’’ anasema Okoth, na
kuongezea:''Tena wanahitaji wawe wakicheza na timu mashuhuri duniani
mara kwa mara. Sio kwamba ni vigumu kufuzu lakini lazima pia serikali
nayo ikubali kutumia fedha kulipia mechi kubwa za kimataifa na tuwe na
msingi mzuri wa kandanda kuanzia mashinani.’’
Origi, mwenye umri wa miaka 19, anasema
amefurahia sana kuchaguliwa kuiwakilisha Ubelgiji kwenye kombe la dunia,
na vile vile kuwa na mshambuliaji mahiri Romelu Lukaku wa Chelsea
ambaye msimu uliopita alichezea Everton kwa mkopo.
''Wachezaji wote wananipa morali sana. Rafiki
yangu Hazard (Eden) na Kompany (Vincent) wameniambia nicheze mchezo
wangu wa kawaida nisiwe na wasiwasi uwanjani,’’ asema Origi aliyecheza
mechi ya mwisho ya kirafiki dhidi ya Tunisia ambayo Ubelgiji ilishinda
kwa bao 1-0. Namuuliza kama ananuia kuhamia England lakini Origi anasema
kwa sasa mawazo yake yote yako Brazil kwa kombe la dunia. Babake Origi
ni shabiki mkubwa wa Liverpool.
Mara ya mwisho Ubelgiji kushiriki kombe la dunia
ni mwaka wa 2002 ambapo kocha wao wa sasa Marc Wilmots alikuwa mchezaji
wa mwisho kuifungia Ubelgiji kwenye kombe la dunia hadi sasa. Wilmots
ana imani na Origi ambaye amechukua nafasi ya Christian Benteke wa Aston
Villa anayeuguza jeraha.
Urusi ndio tisho kubwa kwa Ubelgiji kumaliza
katika nafasi ya kwanza kundi H, na ina motisha wa kufanya vyema kwani
wao ndio wataanda kombe la dunia mwaka wa 2018. Isitoshe Urusi inafunzwa
na kocha anayeaminika kulipwa mashahara wa juu zaidi duniani Fabio
Capello ambaye anaweka kibindoni dola millioni 6.5 kwa mwaka. Matokeo
mazuri zaidi kwa Urusi kwenye kombe la dunia ni mwaka wa 1966
walipomaliza wa nne.
No comments:
Post a Comment