Wauguzi wa hospitali ya mkoa wa Shinyanga wakimuhudumia hakimu Satto 
Nyangoha aliyechomwa kisu shavuni jana, akiwa mahakamani na mlalamikaji 
katika kesi ya wizi wa baiskeli, Emmanuel IzengoHakimu wa Mahakama ya Mwanzo iliyopo eneo la Nguzo Nane, Kata ya Kambarage Mjini Shinyanga, Satto Nyangoha amejeruhiwa kwa kuchomwa kisu katika shavu lake la kushoto baada ya kutoa hukumu ya kesi ya wizi wa baiskeli.
Kitendo hicho kinadaiwa kufanywa na mlalamikaji 
katika kesi hiyo, Emmanuel Izengo (28), mkazi wa Tambukareli, Shinyanga 
baada ya kutokuridhishwa na hukumu iliyotolewa bila ya mshtakiwa, Daniel
 Makelezia, mkazi wa Lubaga Shinyanga na mdhamini wake, Marko Nkelezia 
kuwepo mahakamani.
Katika hukumu yake, Hakimu Nyangoha alisema 
mshtakiwa atakapopatikana atatumikia kifungo cha miaka miwili jela baada
 ya kupatikana na hatia ya wizi wa baiskeli hiyo aina ya Neria yenye 
thamani ya Sh150,000.
Awali, ilielezwa kwamba baada ya tukio hilo la 
wizi lililotokea Agosti Mosi, mwaka huu katika eneo la Nguzo Nane, 
mshtakiwa alikamatwa na kuwekwa mahabusu na kufunguliwa kesi namba 460 
ya 2013 kabla ya kuachiwa kwa dhamana Agosti 23, mwaka huu huku kesi 
yake ikiendelea na pande zote mbili zilitoa maelezo.
Hata hivyo, baada ya kutoa maelezo, si mshtakiwa 
wala mdhamini wake aliyehudhuria mahakamani hapo licha ya kesi hiyo 
kusikilizwa mara mbili bila ya taarifa yoyote kabla ya hakimu huyo kutoa
 hukumu hiyo jana.
Kushambuliwa
Baada ya hukumu hiyo mlalamikaji alitoa shukrani na kuwashika mikono wote waliokuwamo mahakamani humo na kutoka nje.
Ilidaiwa kuwa baada ya dakika 15, Izengo alirudi 
mahakamani hapo na kudai kuwa ameleta risiti ya kumwonyesha hakimu 
thamani ya baiskeli yake alipoingia ndani ndipo kelele za Mshauri wa 
Baraza, Mary Wamba zikaanza kusikika akisema: ‘Njooni jamani hakimu 
kavamiwa anapigwa’.
Baada ya watu waliokuwa karibu kuingia katika 
ofisi ya Mahakama hiyo walikuta hakimu ameshacwhomwa kisu katika shavu 
la upande wa kushoto huku akivuja damu nyingi huku mtuhumiwa huyo 
akiendelea kumshambulia. Baada ya tukio hilo, wasamaria wema walimpeleka
 hakimu huyo katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga ambako alilazwa kwa 
matibabu.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
 Shinyanga, Evarist Mangala alisema mtuhumiwa alikamatwa mara baada ya 
tukio hilo kusubiri hatua za kisheria dhidi yake.
No comments:
Post a Comment