Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chama cha 
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimempitisha Mathayo Torongey 
kuwa 
mgombea rasmi wa ubungekwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mdogo 
wa Jimbo la Chalinze.
Akimtambulisha mgombea huyo kwa Waandishi wa 
habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri wa 
Chadema, John Mrema alisema Torongey alipitishwa juzi na Sekretariati ya
 chama kwa niaba ya kamati kuu.
“Kikao cha Sekretariati kilizingatia maoni na 
ushauri wa wanachama na viongozi wetu wa ngazi za chini, Hivyo kwa kuwa 
hakukuwa na kipingamizi chochote juu ya agombea, chama kilimpitisha 
Torongey” alisema Mrema.
Torongey alishinda kura za maoni za chama hicho 
jimboni Chalinze kwa kupata kura 280 dhidi ya 510 zilizopigwa. 
Aliwashinda wapinzani wake, Omar Mvambo aliyepata kura 84, Francis Mgasa
 61 na Frank Mzoo alijinyakulia kura 23.
Mgombea huyo anatarajia kushindana na Fabian 
Leonard aliyepitishwa na chama cha CUF pamoja na Ridhiwani Kikwete 
anayesubiriwa kupitishwa na kamati kuu ya CCM (CC-CCM).
Mshindi wa uchaguzi huo anatarajia kuziba pengo la
 aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Said Bwanamdogo aliyefariki Januari 22 
mwaka huu.
Mrema ambaye pia ameteuliwa kuwa Mkuu wa 
Operesheni wa Uchaguzi mdogo wa Chalinze, alisema Chadema kina imani 
kubwa na Torongey kushinda uchaguzi wa jimbo hilo unaotarajia kufanyika 
Aprili 6.
Alisema uchaguzi wa jimbo hilo ni muhimu sana kwa 
chama kwa kuwa limeshawahi kuongozwa na Rais Jakaya Kikwete kwa miaka 15
 bila ya kuwa na maendeleo yoyote.
Mrema alisema Chadema hakitishwi na historia ya 
Chama cha Mapinduzi (CCM) ya kuwapitisha baadhi ya watoto wa vigogo 
katika chaguzi ndogo mbalimbali za ubunge zilizowahi kufanyika nchini 
kama njia ya kuwarithi wazazi wao.
Alizitaja chaguzi zile za Arumeru Mashariki ambapo
 CCM kilimpitisha Sioi Sumari kumrithi baba yake marehemu Jeremia 
Sumari, Kalenga; Godfery Mgimwa kumrithi William Mgimwa, na hatimaye 
uchaguzi wa Chalinze ambapo mtoto wa Rais Kikwete, Ridhiwani anatarajia 
kuwania.
Naye aliyekuwa mgombea katika kura za maoni katika
 kinyang’anyiro cha ubunge ndani ya chama hicho, Omari Mvambo alisema 
aliridhishwa na matokeo na mchakato mzima wa uchaguzi.
                
              “Mchakato mzima wa uchaguzi ulienda vizuri na 
wagombea wote tuliridhika na matokeo yalikuwa sahihi. Kwa hiyo nimeamua 
kujidhihirisha kuwa ntampa nguvu mgombea aliyepitishwa kushinda 
uchaguzi,” alibainisha Mvambo
Mgombea aliyepitishwa na Chadema, Torongey alisema kuwa 
anatarajia sifa yake ya uenyeji na historia ya maisha yake duni vitakuwa
 moja ya chachu za kushinda wapinzani wake katika uchaguzi unaotarajiwa 
kuwa na upinzani mkubwa.
Alisema akipata ridhaa ya kuwa mbunge wa jimbo 
hilo, atahakikisha anatatua changamoto za maji, elimu na pia 
kushughulikia masuala ya mgogoro baina ya wafugaji na wakulima uliodumu 
kwa muda mrefu.Mgombea huyo alichukua fomu maalumu ya tume ya uchaguzi 
Mjini Bagamoyo jana ya kugombea ubunge wa jimbo hilo la Chalinze.
credit kwa gazeti la mwananchi
No comments:
Post a Comment