Dodoma. Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji
Frederick Werema amempongeza Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni,
Tundu Lissu, kwa kile alichokiita kuwa ni kuwa na kifua kipana cha
kujali masilahi ya Taifa.
Jaji Werema alimwaga sifa hizo jana muda mfupi baada ya kupitishwa kwa Kanuni zitakazoongoza Bunge Maalumu la Katiba.
Mwanasheria huyo anaungana na wabunge wengine
akiwamo Christopher Ole Sendeka wa Simanjiro (CCM), ambaye mwishoni mwa
wiki alikaririwa akitaka Lissu apewe nafasi ya Waziri wa Katiba na
Sheria kwa sababu ni mahiri katika kusimamia utaifa.
Lissu alikuwa miongoni mwa wajumbe waliopitia na
kuzichambua kanuni hizo ambazo kwa sehemu kubwa, zilizua migogoro
mikubwa wakati zikijadiliwa kabla ya kupitishwa.
“Tufanye kazi ya kukubaliana na kutunga Katiba
yetu, tuache ushabiki wa vyama katika mambo ya msingi kama haya, lakini
nawataka wajumbe waangalie mfano wa Tundu Lissu, si kawaida yake kufanya
mambo ya hekima kama aliyoyafanya lakini amegeuka na kuwa ngome imara
ya maridhiano ya kuzitengeneza Kanuni,” alisema Jaji Werema.
Alisema utaifa na uzalendo ndivyo vilivyomsukuma kufanya kazi hiyo bila ya kuangalia upande mmoja wa chama chake.
Akizungumzia misingi ya Kanuni, aliwataka wajumbe kuvumiliana, kuheshimiana na kupeana nafasi wakati wa kuchangia mijadala.
“Mambo ninayowaomba wajumbe kuyazingatia ni
uvumilivu, werevu, kuacha mambo ya vyama, kusoma alama za nyakati na
kutokuhamaki wakati wa kuchangia,” alisisitiza.
No comments:
Post a Comment