Dodoma, 16.04.2014 
Ndugu Mwenyekiti,
Ndugu Mwenyekiti,
Kamati 12 za Bunge lako tukufu zimeleta Taarifa zake mbele yetu kwa 
ajili ya maboresho ya Rasimu ya Katiba ili kupata katiba inayopendekezwa
 itakayopelekwa kwa Wananchi. Maoni ya Kamati yamegawanyika katika aina 
Kuu 2, maoni ya walio wengi na maoni ya walio wachache. Ndani ya Bunge 
hili majadiliano pia yamekuwa yenye mwelekeo huo huo na kwa kweli hakuna
 majadiliano bali majibizano. Sio afya kwa nchi yetu hata kidogo kuwa na
 Taifa ambalo wawakilishi wake kwenye Baraza nyeti kabisa kama hili 
wanajibizana badala ya kujadiliana, wanabishana badala ya kuongea na 
wanatukanana badala ya kushawishiana.
Imefikia hatua zinatoka lugha za kibaguzi bila kukemeana na badala 
yake tunashangiliana na kupigiana vigelegele. Ubaguzi wa rangi au 
ubaguzi wa aina yeyote ile ni sumu kali dhidi ya umoja wetu na Utu wetu.
 Kauli za kibaguzi, matusi dhidi ya waasisi na dhidi yetu wenyewe ni 
mambo ya kulaani kwa ukali unaostahili.
Ni muhimu kutambua kuwa tofauti na mabadiliko ya katiba yaliyowahi 
kufanyika nchini, mchakato huu wa sasa ni wa kipekee ambao unatoa nafasi
 kwa watanzania wote wa makundi yote kushiriki kwa njia moja ama 
nyingine. Ni wajibu wetu kutambua kuwa kuwa huu ni mchakato shirikishi 
ambao umelenga kuleta maridhiano ya makundi yote ya kisiasa, kijamii na 
kiuchumi na sio kuongeza mgawanyiko uliopo katika jamii yetu. Endapo 
tutafanikiwa kuendesha mchakato huu katika hali ya kuheshimiana, 
kuthaminiana na kwa nia njema sio tu tutaweza kujenga mwanzo mpya wa 
kisiasa wenye kujali umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa lakini pia 
tutaweza kuerejesha imani yao kwa dola, serikali, viongozi na wanasiasa,
 imani ambayo imekuwa ikitoweka na hata kuathiri uhalali wa dola letu 
mbele ya macho na mioyo ya watanzania na kutishia hatma ya taifa letu. 
Mwenendo wa mchakato huu una umuhimu wa kipekee kulinusru taifa letu 
kutoka kwenye dalili mbaya tunazoziona kila siku zikijongea utaifa wetu.
Ndugu Mwenyekiti,
Muungano ni imani. Ni itikadi; ama unaamini katika Muungano au 
huamini katika Muungano. Muungano ni dhana inayoweza kutekelezwa kwa 
muundo wa aina yeyote. Pia ikumbukwe kuwa Muundo wowote unaweza kuvunja 
Muungano iwapo wananchi wa Nchi husika hawautaki.
Hatuoni Nchi ambazo zilikuwa S1 na zimevunjika? Ethiopia iliyozaa 
Eritrea ilikuwa Serikali 1. Somalia iliyozaa Somaliland ilikuwa Muungano
 wa Serikali 1. Malaysia na Singapore zilikuwa Serikali ya Shirikisho na
 zimevunjika. Sudan na Sudan Kusini zilikuwa Serikali 2 na zimevunjika. 
Kila muundo una hatari ya kuvunjika iwapo hakuna matakwa ya dhati ya 
watu kuungana.
Muungano ni imani. Ni itikadi. Maneno ya kusema Serikali 3 zitavunja 
muungano ni maneno ya siasa tu na hayana msingi wa kisayansi. Urusi 
ilivunjika sababu haikuwa na demokrasia na sio sababu ya idadi ya 
Serikali.
Ndugu mwenyekiti,
Rasimu ya Katiba ipo mbele yetu. Tuboreshe. Matusi kwa Tume sio 
jawabu. Vilevile matusi kwa wanazuoni wetu waliobobea sio jawabu. Kero 
za Muungano zilizoainishwa na Tume ni halisia na hakuna walilotunga. 
Lakini pia hofu za kuwa na Serikali ya Muungano dhaifu ni hofu halisi, 
tukibeza tutakuwa mahayawani. Lakini tukitumia hofu hizo kukwepa wajibu 
wa kuboresha Rasimu tutakuwa mazwazwa. Hakuna hoja isiyo na majibu. 
Tukae humu ndani tujibu tutoke na muundo imara.
Ndugu Mwenyekiti,
Kuna hoja ya gharama za kuendesha Serikali ya 3 iwapo tutapitisha 
Rasimu kwa msingi wake huo. Ni hoja ya msingi lakini inajibika. Hivi 
sasa Serikali ya 3 imejificha, ipo. Gharama ni zile zile. Sio lazima 
tuwe na Marais 3, hatujengi ikulu Mpya. Gharama za Wizara za Muungano 
zipo ndani ya Bajeti ya sasa ya Serikali mbili. Hakuna taasisi Mpya 
zaidi ya Tume za uwajibikaji nk. Lazima tuwe na Rais wa Tanganyika? 
Hapana.
Ndugu Mwenyekiti,
Tuwe na Rais 1 tu, Rais wa Jamhuri ya Muungano na Wakuu wa Serikali 
za Washirika watakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Unaweza 
kuwaita unavyopenda lakini Mimi nashauri tuwaite Mawaziri Wakuu na 
watokane na Chama chenye Wawakilishi wengi kwenye Baraza la Wawakilishi 
la Tanganyika na chenye wawakilishi wengi kwenye Baraza la wawakilishi 
la Zanzibar.
Ndugu Mwenyekiti,
Uhuru wa Zanzibar ulipopatikana Zanzibar ilikuwa ‘parliamentary 
democracy’ na vivo hivyo Tanganyika ilipopata Uhuru. Zanzibar 
ilipinduliwa Serikali ya Wazanzibari chini ya Waziri Mkuu Mohamed 
Shamte. Sultan Jamshid alikuwa Mkuu wa Nchi tu (constitutional 
monarchy). Tanganyika kabla ya Jamhuri Mwalimu Nyerere na baadaye Mzee 
Kawawa walikuwa Mawaziri Wakuu. Malkia alikuwa Mkuu wa Nchi. Sasa 
tufanye tuwe na Mkuu wa Nchi mmoja, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa 
Tanzania na Chombo cha utendaji cha Zanzibar na Tanganyika viongozwe na 
Mawaziri Wakuu. Rais mmoja, Nchi moja na Serikali 3.
Hakuna gharama inayoongezeka, mambo ya Muungano yanapungua. Isipokuwa
 katika mambo ya Muungano kwenye Rasimu tuongeze shughuli za uratibu wa 
uchumi, kodi kadhaa na tuwe na masuala ya uratibu (concurrent) kama 
usafiri wa anga, mawasiliano, Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii na Usimamizi
 wa Maliasili za Taifa. Kwa hiyo tuwe na Mambo ya Muungano 
yatakayosimamiwa na Serikali ya Muungano, Mambo yasiyo ya Muungano 
yatakayosimamiwa na Washirika na mambo ya uratibu (concurrent matters) 
yatakayosimamiwa kwa pamoja na Serikali za Washirika na Serikali ya 
Muungano.
Ndugu Mwenyekiti,
Rasimu inapendekeza Muungano wa kisiasa bila Umoja wa Forodha, Soko 
la Pamoja na Umoja wa Sarafu (Monetary Union). Chanzo cha mapato 
kilichopendekezwa na Tume hakitoshi kwa shughuli za Serikali imara ya 
Muungano isiyo egemezi au tegemezi.
Katika mwaka wa fedha 2012/2013 chanzo hiki (tena ushuru wa bidhaa na
 huduma – local and imports) kiliingiza Tshs 1.13 trilioni wakati 
matumizi ya Wizara za Muungano katika mwaka huo wa fedha ilikuwa Tshs 
4.2 trilioni. Katika mwaka 2013/2014 chanzo hiki kinatarajia kuingiza 
Tshs 2 trilioni wakati matumizi ya Wizara za Muungano ni zaidi ya Tshs 
5.3 trilioni. Hivyo ni lazima tuiboreshe rasimu kwa kuongeza vyanzo vya 
mapato ya Muungano ili kuwezesha Serikali ya Muungano kuwa imara, 
inayojitegemea na itakayoweza kuwezesha Serikali za Washirika kutimiza 
wajibu wao wa kutoa huduma kwa wananchi
Turekebishe kwa kuboresha Rasimu maana ni lazima tuwe na sera za 
pamoja za fedha (monetary policy) kama tunataka Muungano imara. Baadhi 
ya hatua hizi zipo tayari ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hivyo 
napendekeza vyanzo vya mapato ya Muungano kuboreshwa ili Dola iweze 
kusimamia Uchumi, navyo ni;
1. Ushuru wa Forodha,
2. Mrahaba wa uvunaji wa Rasilimali za Nchi,
3. Ushuru wa Bidhaa na Huduma zilizozalishwa nje ya Tanzania,
4. Mapato kutoka kwenye kampuni za kibiashara za Serikali ya 
Muungano, Mamlaka za Usimamizi zenye maduhuli, maduhuli kutoka Wizara za
 Serikali ya Muungano na Gawio la Benki Kuu ya Tanzania.
Ndugu Mwenyekiti,
Mapato haya haya ya sasa yanaweza kugawanywa kwenye Muundo wa 
Serikali 3 na tusiongeze kodi hata senti moja na Muundo Mpya ukafanya 
kazi. Hatuhitaji Tshs 3 trilioni za ziada kwa ajili ya Serikali Mpya. 
Bajeti ya Serikali ya mwaka huu wa fedha 2013/2014 ni shilingi 18 
trilioni, kati ya hizo mapato ya ndani ni shilingi 11 trilioni na katika
 mapato hayo ya ndani shilingi 10 trilioni ni kodi. Gharama za kuendesha
 Wizara za sasa za Muungano ni tshs 5.6 trilioni lakini kati ya hizi 
Tshs 3.3 trilioni malipo ya Deni la Taifa. Hakuna trilioni 3 za ziada, 
za kazi gani? Hata kama fedha hizo zikihitajika, zisitutishe maana zipo.
Hatuhitaji kuongeza kodi, tunahitaji kuondoa ubadhirifu na kudhibiti 
matumizi yasiyo ya lazima. Tunapoteza Mapato lukuki kwenye misamaha ya 
kodi (theluthi ya mapato ya idara ya forodha inasamehewa, sawa na Tshs 2
 trilioni kwa mwaka), ukwepaji wa kodi (asilimia 5 ya Pato la Taifa 
inapotea, sawa na Tshs 2.3 trilioni kwa mwaka ) na ubadhirifu mwingine 
uliokithiri. Hivyo udhibiti wa asilimia 50 tu wa misamaha ya kodi na 
ukwepaji kodi unaongeza mapato zaidi ya trilioni 2 ambazo Serikali ya 
Muungano inaweza kugawa kwa Washirika kwa miradi maalumu ya kitaifa. 
Hivi sasa kamati ya PAC (Ya Bunge la Jamhuri ya Muungano) imeanza 
utaratibu wa ukaguzi wa misamaha ya kodi na kuweka wazi kwa umma ukaguzi
 huo ili kudhibiti misamaha holela. Vilevile kwa kibali maalumu cha 
Spika wa BUNGE, PAC imeanza uchunguzi (an inquiry) kuhusu ukwepaji kodi 
unaofanywa na makampuni ya kimataifa. Hizi ni juhudi za kuongeza mapato 
mpaka kufikia uwiano wa 25% ya mapato ya kodi kwa GDP (tax GDP ratio).
Ndugu Mwenyekiti,
Serikali 3 zitaweka Uwazi wa Mapato na zitaweka Uwajibikaji kwa 
serikali kutazamana zenyewe. Hizi za sasa zimejaa lawama sababu hakuna 
Uwazi. Naomba kuuliza, fedha za mapato kutoka TCRA lini zimeenda 
Zanzibar? Mawasiliano ni jambo la Muungano. Lini fedha za TCAA zimeenda 
Zanzibar? Gesi Asilia ni jambo la Muungano, hivi Zanzibar wanapata mgawo
 wa asilimia ngapi kutoka gesi ya Songosongo? Anga ni jambo la Muungano,
 fedha za chenji ya rada zimerudi, Zanzibar imepata kitabu hata kimoja? 
Mimi ni mwenyekiti wa PAC, najua haya ninayosema na hamtayamaliza katika
 S2 sababu ya confusion ya Muundo. Tatu ni Muundo unaoeleweka. Tukiamua 
zifanye kazi zitafanya.
Ndugu Mwenyekiti,
Hoja ya gharama isitumike kutisha wananchi kwa sababu ni hoja ‘very 
relative’ na ninashangaa sana kuona baadhi ya wasomi, wachumi wanaongea 
suala hili bila kutafakari kwa kina. Unaweza ukawa na Serikali 1 ukawa 
na gharama kubwa zaidi kuliko Serikali nne. Gharama za kuendesha 
shughuli za usalama zitakuwa nafuu zaidi kwenye Serikali 3 kuliko 
Serikali 2 kwani kwenye Serikali 3 kila mtu atakuwa amefurahi, ndani ya 3
 kuna 2 na 1. Zikiwa mbili, wa 3 watanuna maana ndani ya 2 hakuna 3. 
Watu wote wakiwa na furaha vitendo vya uhaini dhidi ya Dola vinapungua. 
Lakini Muungano ukivunjika gharama za Ulinzi wa nchi zote mbili zitakuwa
 kubwa sana na lazima mabeberu wataingia kati upande wa mmoja wetu. 
Hivyo nashawishi wajumbe tuulinde Muungano wetu kwa kuufanyia 
marekebisho makubwa ya kimuundo na kuunda Chombo kingine cha utendaji 
kwa masuala yasiyo ya Muungano ya Tanganyika.
Muungano kuvunjika?
Ndugu Mwenyekiti,
Kuna ambao wanaamini kabisa kwamba kuifukua Tanganyika ndani ya 
Muungano kutavunja Muungano na hivyo wanataka S2 ziboreshwe. Kuna ambao 
wanataka S2 kwa kufuata mkumbo tu na kwamba ni ‘sera’ ya chama chao.
Kuna ambao wanaamini kabisa kwamba S3 ndio njia ya kuimarisha 
Muungano na kuufanya endelevu kwa kuweka uwazi katika muundo wa Muungano
 na usawa wa Washirika. Kuna ambao S3 ni njia ya kutokea kuelekea 
kuvunja Muungano maana ama hawaamini katika muungano au hawana itikadi 
yeyote (ideological bankruptcy).
Wanaong’ang’ania S2 wakidhani wanalinda Muungano watambue kuwa wanawapa nguvu S3 wanaotaka kuvunja muungano.
Ni busara na maono ya mbali kwamba wale wanaoupenda Muungano 
(ideologically clear people) kuhakikisha S3 zenye Serikali imara ya 
muungano. Usipotaka mabadiliko, mabadiliko yatakutaka wewe.
Nataka Muungano. “I am a Unionist.” Lakini nataka Muungano 
unaoeleweka, wenye uwazi na uwajibikaji. Muungano wa usawa. Muungano 
endelevu.
Mimi ni Mtanzania.

No comments:
Post a Comment