“Sote tuwe na Umoja” (rej. Yn 17:21)
UTANGULIZI:
wapendwa, 
tunapohitimisha kipindi cha Kwaresima kilichokuwa na ujumbe: “Ukweli 
utawaweka huru” (Yn. 8: 32), tunawaletea ujumbe wa “Umoja” ili kuongeza 
msisitizo kwenye ujumbe wetu wa Kwaresma. Tunaitwa kukubali kuwa umoja 
ni ukweli msingi wa kila mafanikio ya jumuiya ya mwanadamu.
Ufufuko ni 
Pasaka inayomaanisha kivuko au kupita kwa Wayahudi toka kwenye matatizo 
ya utumwa hadi uhuru kamili. Kwa Wakristo ni kuvuka kutoka utumwa wa 
fikra za kifo (dhambi) hadi uhuru kamili wa ufufuko wetu na Bwana Yesu. 
Kwahiyo, furaha za Pasaka zinapaswa kusheheni shukurani za dhati kwa 
zawadi nyingi alizotujalia Mungu Muumba wetu tokea mwanzo na hasa 
nyakati hizi katika mwanga wa Ufufuko wa Kristo. Adhimisho la Pasaka 
litawaliwe na furaha, amani na matumaini makuu yaliyoletwa kwa Ufufuko 
wa Bwana wetu Yesu Kristo. Mtume Paulo anatuambia: “Mungu na ashukuriwe 
atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo” (1Kor. 15:57).
Wakati 
dhambi na kifo husababisha kujitenga; uhuru, furaha na amani husababisha
 kuungana. Ndivyo ilivyotokea kwa Adamu na Eva. Walipokuwa bila dhambi 
walikuwa huru, wenye furaha, amani na umoja na Mungu. Walipotenda dhambi
 walimkimbia Mungu, wakatafuta kujificha. Hata wao wenyewe walioneana 
aibu na hatimaye wakafukuzwa kutoka kwenye bustani ya Edeni (Mwa. 2:25; 
3:7-8, 23-24).
1.Ndugu zetu
 katika Kristo, “Amani iwe Kwenu” (Yn. 20:19). Wakati huu wa Pasaka, 
wakati ambao pia mchakato wa kuandika Katiba ya nchi yetu unaendelea, 
hatuwezi kuacha kutafakari kwa dhati juu ya umoja wetu sisi Watanzania. 
Bila shaka, moja ya mihimili mikubwa ya umoja wa kitaifa ni uongozi 
bora.
Mwenyezi 
Mungu aliwatoa watu wake utumwani Misri na kuwaweka huru kwa kuwateulia 
viongozi miongoni mwao. Kiongozi wa kwanza alikuwa Musa (Kut. 3:10).
• Chini ya 
uongozi wa Musa Wayahudi walichukua muda mrefu kujenga umoja na uelewa, 
kwamba walikuwa watu wa Mungu na walipaswa kumtambua kiongozi wao kama 
mteule wa Mungu (Kut. 16:3; 17:4.
• Katika 
kutangatanga kwao jangwani, iliwachukua pia muda mrefu kutambua uovu wao
 na kujitakasa dhidi ya dhambi zao (Kut. 32:1-14).
• Hata 
wakiwa tayari katika nchi waliyoahidiwa hawakuacha machukizo yao kwa 
Mungu pamoja na kukanywa mara kwa mara na Manabii wake Mwenyezi Mungu 
(Amu. 2:11-13).
Wakati ulipowadia, Mungu alimtuma Mwanae Yesu Kristo kujenga Utawala wa Mungu juu ya msingi wa imani na ukweli (Gal. 4:4):
• Imani kwa Mungu na imani baina ya watu wenyewe – kuaminiana – ndio msingi wa Utawala wa Mungu (2Thes. 2:13-17).
• Lakini 
kutokana na udhaifu wa kibinadamu, mara nyingi tunavunja umoja wetu na 
Mungu na kati yetu wenyewe kwa kiwango cha kutotaka kuishi pamoja; 
tunabaguana na hatutendeani haki (Mwa. 4:7-8).
Katika 
ulimwengu wa leo, tunashuhudia madhara ya utengano wa namna nyingi. 
Dhambi nyingi za binadamu zinasababisha mifarakano na vita. Hayo ni 
matukio ya kila mara katika nchi nyingi ulimwenguni na hasa kwetu 
Afrika. Hata historia yetu wenyewe ina matukio mengi ya jamii kufarakana
 na kujizamisha katika vita.
• Mababu 
zetu walipitia maisha marefu ya kuhamahama na kuchukuliwa utumwani na 
wengine kubaki watwana na watawaliwa wa kikoloni kwa vipindi virefu 
kabla ya kujipatia uhuru wa kujitawala.
• Tulipopata uhuru, tulijifunza kujenga umoja katika tofauti zetu kubwa za kikabila na kufikia taifa moja.
• Tulichukua
 hatua kubwa kuunganisha nchi mbili huru, Tanganyika na Zanzibar, na 
kuifanya kuwa nchi moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa 
kielelezo kwa Bara la Afrika cha kujenga umoja.
2.Hatua zote
 hizo tulizopitia na tulizochukua kwa makusudi kabisa, tulikuwa na nia 
na utashi wa kuwa wamoja. Tulitaka kujenga maendeleo ya pamoja na 
mafanikio ya kila Mtanzania kufikia maisha bora. Jitihada hizi njema 
zimekuwepo kwa miaka hamsini iliyopita. Tumefanikisha mambo mengi katika
 umoja wetu ambao unatusukuma kumshukuru Mungu. Kwa muda mrefu umoja wa 
Watanzania umeonekana kwa mataifa mengine kuwa ni kielelezo cha umoja wa
 kitaifa wa hali ya juu sana. Ni umoja uliokua kufikia kiasi cha kufuta 
tofauti za awali za mataifa yaliyohusika kuunda umoja.
Tunamshukru 
mwenyezi Mungu kwa kuifanya Nchi yetu kuwa kimbilio la waliokata tamaa. 
Tanzania imewapa wakimbizi mahali salama pa kuishi pamoja na Watanzania.
 Chini ya Jamhuhuri ya Muungano wa Tanzania, waliokuwa bado chini ya 
wakoloni, waliandaliwa kujikomboa na kuwa mataifa huru.
Pamoja na 
mafanikio hayo makubwa, zimejitokeza dosari kadhaa katika umoja 
zilizofanya umoja wetu upoteze baadhi ya sifa zake za awali. Kupungua 
kwa hisia za kujisikia watu wote ni taifa moja, ni dosari iliyoanza 
kukua taratibu na sasa inaonekana kuwa ndio ukweli. Baadhi ya Watanzania
 wanafikiri kuwa umoja unaofuta tofauti haufai ila umoja unaosisitiza 
tofauti kama ulivyo umoja wa kikanda (kama ilivyo SADC, ECOWAS, n.k) 
ndio unafaa! Wakati mataifa mengine yanatamani umoja unaofanana na ule 
umoja wetu wa awali, baadhi yetu tunatamani kurudi nyuma kwenye umoja wa
 mpito!
Kutokana na 
mapungufu yaliyodhihirika ndani ya mafanikio yetu, umuhimu wa kufanya 
marekebisho ulidhihirika. Ni kwa sababu hiyo, watu wengi walitaka na 
wanataka mabadiliko au mageuzi ya msingi sana. Kwa msukumo huo ndio 
sababu tuliingia katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya.
3.Kazi ya 
kuandika Katiba si nyepesi na yataka umakini mkubwa. Haishangazi sana 
tunapojionea mivutano na migongano ya hoja kutoka kwa makundi kinzani 
katika nchi moja. Mawazo ya wengi yamewasilishwa kisheria na Tume ya 
Mabadiliko ya Katiba kwa ajili ya kujadaliwa na Bunge Maalum la Katiba 
(BMK). Sasa, tunashuhudia makundi yenye nguvu yakijaribu kushinikiza 
kuingizwa matakwa yake kwenye Katiba kwa njia zozote zile ili 
kujihakikishia kuendelea kulinda maslahi yake ya kisiasa. Wajumbe wa 
Bunge Maalum Katiba wanazozana, wanakashifiana,wanatukanana na hawataki 
kuachana na itikadi za kisiasa ili kufikia muafaka katika masuala muhimu
 yatakayowahakikishia raia wa kawaida kushiriki kwenye fursa za 
maendeleo kwa manufaa ya wote. Hayo lakini yasitukatishe tamaa na 
kujiona kama tu watu wa kushindwa wakati tukiwa bado kwenye mchakato 
mrefu wa kujipatia jukwaa jipya kwa mustakabali wa taifa letu Tanzania.
Tushirikiane
 na wote wenye nia njema kupambana na nguvu za maovu na ubinafsi na 
kuachana na itikadi za kisiasa na matakwa ya kiuchumi ya matabaka ya 
walio nacho ili kupigania haki za wanyonge. Tuandae Katiba ambayo 
itatupatia misingi imara ya maadili itakayotuongoza kupigana dhidi ya 
ubinafsi na ufisadi, na kutetea haki za binadamu kwa wote. Vigezo vyote 
muhimu kwa maisha ya mshikamano kitaifa vimeandikwa katika Rasimu ya 
Katiba Sura ya 1 hadi ya 5. Tukisha kukubaliana na yaliyomo katika sura 
hizo, muundo wowote wa Serikali unawezekana kwa kuzingatia kanuni za 
uwiano wa madaraka na wajibu wa mihimili mitatu ya Dola kwa mujibu wa 
Sura za 8 hadi 15.
Ili tufikie lengo letu la kuwa na Katiba bora katika hatua tuliyofikia ya mchakato wa Katiba Mpya yatubidi kuzingatia yafuatayo:
• Kuheshimu kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuitumia kama ilivyokusudiwa na sheria iliyoiweka.
• Kuwa na nia njema ya kweli ya kutafuta suluhisho la matatizo mengi ya utendaji katika Dola zilizopo katika Muungano.
• Kuwa na 
hamu ya kujitoa kwa taifa na kulitumikia kwa moyo bila kutawaliwa na 
ubinafsi au kujipendelea kiinchi na kiukanda kwa madhumuni ya kuboresha 
maisha ya Watanzania wote.
• Chaguo la 
muundo wa Dola, sharti liongozwe na malengo na madhumuni ya umoja wetu 
wa kutaka tuishi kwa mshikamano wa dhati. Uchaguzi wa muuungano wa 
serikali moja, mbili au tatu sharti ufanywe kwa dhamiri safi iliyo na 
uelewa uliochambua matatizo yaliyopo ya Muungano na kuridhia mfumo 
utakaosuluhisha matatizo hayo pasipo mashaka yoyote.
4.Baada ya 
kutafakari historia ya ukombozi wa mwanadamu kwa ufupi na hatua 
Watanzania tuliyofikia katika uhuru wetu wakati huu wa adhimisho la 
Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo mwaka 2014, tungependa kwa namna ya 
pekee kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumvuvia Rais Jakaya M. Kikwete 
ujasiri wa kuamua kuanzisha mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya Jamhuri 
ya Muungano wa Tanzania kisheria katika wakati muafaka.
Kwa mchakato
 huo wa Katiba, kupitia Tume yake Huru, Watanzania wamepata fursa ya 
kusema kila jambo lililowaelemea maishani na kuainisha namna wanavyotaka
 kujitawala. Wakati ulikuwa mwafaka kwa sababu kulikuwa na manung’uniko 
mengi ya ukiukwaji wa Katiba ya sasa ambayo hayakuweza kujibiwa na 
Serikali zilizopo. Hatua ya kuamua kuyakabili hayo kwa sheria ya 
Kurekebisha Katiba iliwapa wananchi fursa ya kutoa maoni yao bila mizozo
 na machafuko.
5.Tume ya 
Mabadiliko ya Katiba imewasilisha kwenye Bunge Maalum la Katiba Rasimu 
ya Katiba iliyotokana na maoni huru ya watu binafsi na makundi mbali 
mbali zikiwemo taasisi za dini, mamlaka za kiserikali na asasi huru za 
kiraia. Tunalisihi na kulishauri Bunge Maalum la Katiba kuheshimu mawazo
 yaliyowasilishwa na kutumia busara zilizopendekezwa za kujenga muundo 
wa Muungano utakaokidhi mahitaji ya utangamano, mshikamano, amani, 
maadili, uhuru na uwajibikaji wa viongozi na raia wa Tanzania.
HITIMISHO
Ndugu wapendwa,
Wakati huu 
wa Pasaka, tuendelee kuliombea Bunge Maalumu la Katiba ili wajumbe wawe 
wazingatifu wa matakwa na matarajio ya Watanzania yalivyoainishwa katika
 Rasimu ya Pili ya Katiba na Tume ya mabadiliko ya Katiba kwa kuheshimu 
maoni ya Watanzania na kuboresha maoni hayo kwa hekima na busara ili 
kulinda mstakabali wa Taifa letu; Tanzania yenye amani kwa ustawi wa 
watu wote.
“Ingekuwa heri leo msikie sauti hii; msifanye migumu mioyo yenu”. (rej. Zab 95:7-8)
Tuombe:
Ee Bwana, 
katika upendo wako uwape neema watu wa taifa lako, waishio Tanzania. 
Katika upendo wako ujenge tena nguzo za imani, matumaini na mapendo 
katika mji nchi yetu. Watanzania wakiwa na imani, matumaini na mapendo 
ya haki utapendezwa na sadaka wakutoleazo; kila mtu akijitolea yeye 
mwenyewe kwako kama sadaka safi juu ya altare, pamoja na katika Kristo 
Mfufuka aliye katika Ekaristi.
Mama Bikira 
Maria atuombee ili ndani yetu uzaliwe upya uaminifu unaotupa uwezo wa 
kutangaza kazi kuu ya Mungu. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana 
wetu. Amina.
Amani ya Kristo Mfufuka iwe nanyi
Ni sisi Maaskofu wenu:
1. Mhashamu Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Askofu wa Iringa
2. Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Dar es Salaam
3. Mhashamu Askofu Mkuu Josaphat Lebulu, Arusha
4. Mhashamu Askofu Mkuu Paul Ruzoka, Tabora/Kigoma Msimamizi
5. Mhashamu Askofu Telesphor Mkude, Morogoro
6. Mhashamu Askofu Gabriel Mmole, Mtwara
7. Mhashamu Askofu Mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi, Ofm Cap, Mwanza,/Shinyanga
8. Mhashamu Askofu Bruno Ngonyani, Lindi
9. Mhashamu Askofu Anthony Banzi, Tanga
10. Mhashamu Askofu Agapiti Ndorobo, Mahenge
11. Mhashamu Askofu Evaristo Chengula, IMC, Mbeya
12. Mhashamu Askofu Augustino Shao, Cssp, Zanzibar
13. Mhashamu Askofu Damian Kyaruzi, Sumbawanga
14. Mhashamu Askofu Severine NiweMugizi, Rulenge-Ngara
15. Mhashamu Askofu Desiderius Rwoma, Bukoba /Singida Msimamizi
16. Mhashamu Askofu Method Kilaini, Bukoba
17. Mhashamu Askofu Damian Dallu, Geita/Askofu Mkuu Mteule Songea
18. Mhashamu Askofu Ludovick Minde, OSS, Kahama
19. Mhashamu Askofu Alfred Leonard Maluma, Njombe
20. Mhashamu Askofu Castor Paul Msemwa, Tunduru-Masasi
21. Mhashamu Askofu Beatus Kinyaiya, Ofm Cap, Mbulu
22. Mhashamu Askofu Michael Msonganzila, Musoma
23. Mhashamu Askofu Issac Amani, Moshi
24. Mhashamu Askofu Almachius Rweyongeza, Kayanga
25. Mhashamu Askofu Rogath Kimaryo, Same
26. Mhashamu Askofu Salutaris Libena, Ifakara
27. Mhashamu Askofu Eusebius Nzigilwa, Dar es Salaam
28. Mhashamu Askofu Renatus Nkwande, Bunda
29. Mhashamu Askofu Gervas Nyaisonga, Mpanda /Dodoma
30. Mhashamu Askofu Bernadin Mfumbusa, Kondoa
31. Mhashamu Askofu John Ndimbo, Mbinga
32. Mhashamu Askofu Titus Mdoe, Dar es Salaam

No comments:
Post a Comment