TUME ya Uchaguzi nchini (NEC) inadaiwa kuingia katika mchakato wa 
mwisho wa kuzipa zabuni ya kuandaa vifaa vya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 
kampuni za M/S Jazzmatrix Cooperation na M/S Invu IT Solution 
zinazodaiwa kuwa na rekodi mbaya ya utendaji.Tanzania Daima limedokezwa kuwa mkakati huo unahusishwa na  njama za 
kutaka kukibeba Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi huo kwa 
kuchakachua matokeo ya kukibakiza madarakani.
Kampuni hizo ambazo katika zabuni ya Tume ya Uchaguzi zimetajwa 
kushirikiana na Kampuni ya Kitanzania ya M/S SCI Tanzania Limited, mbali
 ya kutojulikana zinapotoka, pia ndizo zimekuwa na gharama kubwa kuliko 
kampuni nyingine zilizoomba kazi hiyo.Kiwango ambacho kampuni hizo zilitaja na kukubaliwa na NEC kwa ajili 
ya kuandaa vifaa vya kielektroniki vya kusajili wapiga kura (Biometric 
Voters Registration) ni zaidi ya euro milioni 60, sawa na sh bilioni 
126.3, wakati kampuni zinazofuata zikihitaji kuanzia euro milioni 40.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), 
Zitto Kabwe, ni mmoja wa viongozi waliofichua mkakati huo, akidai 
unafanywa na serikali ya CCM ili kuhakikisha wanajiandaa kudhibiti kila 
eneo ili waweze kubaki madarakani. Alisema lengo ni kuhakikisha mchakato wa vitambulisho vya kupigia 
kura vya kielektroniki vina kuwa na faida kwa CCM na kukiingizia fedha 
chama hicho za kutumia kwenye uchaguzi huo kupitia mfumo huo dhaifu wa 
vitambulisho hivyo.
Zitto alisema kutokana na hali hiyo, amemwandikia Mdhibiti na Mkaguzi  Mkuu wa Serikali (CAG) barua ya kutaka
 ukaguzi wa zabuni hiyo ufanyike kwa kushirikisha Taasisi ya Kuzuia na 
Kupambana na Rushwa (Takukuru) na vyombo vingine vya usalama kwa ajili 
ya kujiridhisha.
“Wenzetu CCM wanafanya mikakati ya kujiandaa na Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kuhakikisha wanapata fedha za kutosha na hata
 mazingira mabaya ya vifaa vitakavyotumika katika upigaji kura na sasa 
wameshaingia hata katika Tume ya Uchaguzi kwa ajili ya kutengeneza 
mazingira,” alisema Zitto.
Aliongeza kuwa kiasi kilichotolewa ni kodi ya Watanzania na kwamba ni
 vema taifa likajiridhisha kuwa matatizo yaliyotokea Kenya na Ghana 
hayatajirudia Tanzania, hasa wakati wa upigaji kura.
Gazeti hili limeona barua hiyo ya Zitto kwenda kwa CAG, ya Novemba 7,
 2013, yenye kichwa cha habari; ‘Zabuni ya Biometric Voters Registration
 (BRV KITS) No. IE/018/2012-13/HQ/G/19 yenye thamani ya sh bilioni 
126.3.’
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini anasema kuwa NEC imekuwa katika mchakato wa zabuni tajwa hapo juu. “Zabuni hiyo sasa imeanza kuleta malalamiko miongoni mwa wananchi 
kutokana na kinachosemekana kuwa kampuni iliyopewa zabuni hiyo haina 
uwezo kiteknolojia, pia bei zao ni kubwa. “Katika mafunzo ya hivi karibuni ya SADCOPAC jijini Nairobi 
tuliazimia kuwa ni vema kwenye zabuni nyeti kama za namna hii, SAIs wawe
 na uwezo wa kufanya ukaguzi kabla ya zabuni kutolewa na kuanza 
kutekelezwa,” alisema.
Kwa mujibu wa nyaraka za NEC ambazo Tanzania Daima linazo, kampuni 
zilizopewa tenda ya pamoja yenye kugharimu kiasi cha dola 78, 
987,636.00, sawa na sh 126,291,375,455 ni M/S Jazzmatrix Cooperation na 
M/S Invu IT Solution ambazo hazijulikani nchi zinapotoka zikiwa 
zinashirikiana na M/S SCI Tanzania Limited.
Katika nyaraka hizo kampuni zilizokosa tenda na ambazo zimelalamika 
kwa Mkurugenzi wa NEC namna mchakato wa kutoa zabuni hiyo ulivyoendeshwa
 zimeainishwa kuwa ni M/S Zetes SA ya nchini Ubalgiji, M/S IRIS 
Corporation Technology ya Malaysia, M/S Lithotech Exports ya Afrika 
Kusini, M/S Safran Morpho ya Ufaransa na M/S Avante International 
Technology, Inc ya Marerkani.
Kampuni hizo zinahoji njia na sababu zilizowafanya wakose tenda hiyo 
licha ya kuwa na uzoefu, vifaa bora pamoja na kuwa na kiwango kidogo cha
 gharama tofauti na kampuni iliyopewa kazi.
Katika moja ya malalamiko yao, Kampuni ya M/S Morpho, inalalamika 
kutofahamishwa namna walivyokosa vigezo vya kupata kazi hiyo licha ya 
kuwa na sifa za kimataifa za kufanya kazi huku ikiwa imetoa bei nafuu 
kuliko kampuni iliyopata kazi.“Tulikuwa miongoni mwa washindani muhimu kwa kuwa kiwango chetu 
kilikuwa ni sh bilioni 97.8 ambazo ni sawa na euro 44,939,912 + sh 
3,843,736,140.“Ujuzi, vigezo na uzoefu wetu havilingani, duniani kote tumefanya 
kazi katika maeneo mengine kwa ufanisi na tunashindwa kuelewa kivipi 
walishinda hao ambao wamepata kazi kwa kiwango cha zaidi ya sh bilioni 
27.8 ikilinganishwa na yetu,” ilisomeka sehemu ya barua.
Alipotafutwa Mkurugenzi wa NEC, Julius Mallaba, alisema hawezi 
kuliongelea suala hilo katika simu na kuomba mwandishi awasiliane na 
Kaimu Mkurugenzi wa NEC, Dk. Sist Cariah, ambaye alisema mchakato wa 
kupata kampuni ulifuatwa kisheria. Dk. Cariah alisema si kweli kwamba kampuni iliyopewa kazi haina uwezo
 bali malalamiko yanatoka kwa watu walioshindwa kupata kazi hiyo.
Alipoulizwa juu ya uzoefu wa kampuni hiyo na wapi ilifanya kazi, Dk. 
Cariah alisema kwa maelezo waliyonayo ni kwamba kampuni hiyo ina uzoefu 
wa miaka 35 wa kufanya kazi, huku akishindwa kuainisha sehemu ilizowahi 
kufanya kazi.
Kuhusu wapi zimetoka kampuni hizo, Dk. Cariah alisema suala la 
kutoainishwa kimaandishi ni makosa ya kawaida, huku akitaja kuwa 
zinatoka katika nchi ya India na Australia.
Kuhusu gharama, Dk. Cariah alisema licha ya makampuni mengine kutaja 
gharama za chini, zingeweza kuwa na gharama kubwa zaidi wakati wa 
kukamilisha kazi hiyo kutokana na kuwa na gharama zilizojificha.
Source Tanzania Daima

No comments:
Post a Comment