Dar es Salaam. Hatimaye watumishi waliokuwa wakitafutwa kujaza
nafasi 70 za mkaguzi msaidizi wa uhamiaji wamepatikana baada ya usaili
mzito uliohusisha zaidi ya watu 6,000 kati ya zaidi ya watu 10,000
walioomba nafasi hizo.
Watumishi hao wapya wanatakiwa kuripoti makao
makuu ya Idara ya Uhamiaji Julai 29, mwaka huu, ikiwa ni mwezi mmoja
baada ya kuchujwa kutoka idadi ya watu 6,115 waliofanya usaili kwenye
Uwanja wa Taifa jijini hapa.
Awali, Idara ya Uhamiaji iliwaita watu 10,800 katika usaili lakini hawakufika wote.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Isack
Nantanga baadaye alibainisha kuwa baada ya usaili wa watu 6,115,
walipatikana 1,681 ambao waliingia katika kinyang’yiro cha kusaka
watumishi 70 waliotajwa jana.
Majina ya washindi hao yaliwekwa bayana katika
taarifa ya katibu mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Mbarak Abdulwakil
ambaye amewataka watumishi hao wapya wafike kwa wakati.
Taarifa hiyo iliyotolewa kupitia vyombo vya habari
jana ilisema; “Ni muhimu kufahamu kuwa uchaguzi wa walioitwa kwenye
ajira umezingatia vipaumbele vya idara na kutoa nafasi kwa waombaji
kutoka Zanzibar, ufaulu kuanzia alama ya asilimia 50 na kuendelea pamoja
na jinsia,” ilisema taarifa hiyo.
Usaili huo wa aina yake umebaki kuwa gumzo huku
baadhi ya wachambuzi wa masuala ya uchumi na ajira wakitaja kuwa ni
dalili za wazi kuwa bomu la ukosefu wa ajira linakaribia kulipuka.
Kundi la wasaka ajira hao lilijumuisha vijana wenye umri kati ya miaka 22 na 30.
No comments:
Post a Comment