VIONGOZI
na Wanachama wapatao 50 wa Klabu ya Simba Jana walitembelea eneo la
mradi wa uwanja wao ulioko Bunju ‘B’ jijini Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo, Wanachama hao
walifanya kazi ya kulisafisha eneo hilo kwa kufyeka ikiwa ni hatua za
awali za kutaka kuuendeleza, ambalo linakadiriwa kuwa na eka 25.
Lengo la kufanya ziara pamoja na
kusafisha eneo hilo ni mkakati wa klabu hiyo, kutaka kuanza rasmi
mipango ya uendelezaji wa eneo hilo.
Eneo
hilo linatarajiwa kujengwa uwanja wa mpira utakaokuwa ukimilikiwa na
klabu hiyo, pamoja na majengo mengine muhimu yatakayoendana na sura ya
kimichezo.
Katika hatua za awali, klabu hiyo
imepanga kufyeka pamoja na kupitisha greda lengo likiwa ni kusafisha
eneo hilo tayari kwa ujezi wa uwanja utakaoweza kutumiwa na timu yake
kwa ajili ya mazoezi na mechi nyingine za kirafiki.
Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga,
ameahidi mpaka kufikia Aprili mwaka huu eneo hilo litakuwa na sura ya
kiwanja cha michezo huku jitihada zingine zikiendelea kufanywa na
Uongozi kwa ajili ya mradi mkubwa wa kituo hicho ambacho hapo baadaye
utahusisha hosteli ya wachezaji, mgahawa, gym pamoja na bwawa la
kuogelea.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, mpango wa awali utahusisha kuzungusha uzio eneo lote pamoja na ujenzi wa uwanja wa kuchezea mpira.
Kamwaga alisisitiza mradi wa ujenzi
mkubwa wa eneo hilo bado unafanyiwa kazi na uongozi wa klabu hiyo ili
kumpata mkandarasi atakayesimamia ujenzi huo na mipango itakapokuwa
tayari basi itawekwa wazi isipokuwa kwa sasa wanachofanya ni hatua za
awali za uendelezaji wa eneo hilo.
Asha Muhaji
Ofisa Habari
Simba Sports Club
No comments:
Post a Comment