Jana tarehe 29 Julai, 2014 nimefanya mahojiano katika kipindi cha
PowerBreakFast kinachorushwa na Clouds FM. Baadhi ya vyombo vya habari
vimeandika mahojiano yale. Napenda nitoe ufafanuzi kidogo kuhusu msimamo
wangu kuhusu mchakato wa Katiba.
Kwanza, Mimi sijawahi kuwa UKAWA wala kundi lolote lile katika Bunge Maalumu la Katiba
isipokuwa kundi linalotaka maridhiano. Msimamo wangu kuhusu Muungano ni
Serikali Tatu Zilizoboreshwa (S3z) ili kuwa na Muungano imara usio
tegemezi wala egemezi kwa Washirika wake.
Pili, Mimi niliunga mkono ‘protest’ ya baadhi ya Wajumbe wa Bunge
Maalumu la Katiba kupinga lugha za matusi na lugha za kibaguzi
zilizokuwa zinaendelea ndani ya mkutano ule. Vilevile niliunga mkono
kwamba Rasimu inayopaswa kujadiliwa ni Rasimu iliyotokana na Tume ya
Marekebisho ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Sinde Warioba.
Nasisitiza umuhimu wa kupata Katiba BORA itakayoimarisha DOLA ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
Tatu, kwa hali ya sasa kuna mkwamo katika kupatikana kwa Katiba Bora.
Mkwamo unaotokana na kutokuwepo kwa nia ya dhati ya kupata maridhiano
ya pande zinazopingana. UKAWA hawataki mazungumzo na Viongozi wa Bunge
la Katiba badala ya kujenga maridhiano kila siku wanawabeza UKAWA jambo
ambalo kamwe haliwezi kujenga mwafaka. Ushauri wangu ni kuahirisha
mchakato mzima wa kuandika Katiba mpaka mwaka 2016 baada ya Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2015. Katiba ya sasa ifanyiwe marekebisho machache kama
ifuatavyo;
i) Tume ya Uchaguzi ili iwe huru na ionekane kuwa huru, ikiwemo
kuwaondoa watumishi wa Halmashauri za Wilaya, Miji na Majiji katika
kusimamia uchaguzi
ii) Kuruhusu mgombea binafsi
iii) Kuondoa Mafuta na Gesi kama Jambo la Muungano ili Zanzibar ianze
mara moja kusimamia kwa uhuru utafutaji wa Mafuta katika vitalu
vilivyopo upande huo wa Muungano
Mkutano wa Bunge Maalumu utakaofanyika bila kuwepo kwa maridhiano
utakuwa hauna maana yeyote na itakuwa ni sawa na kupoteza muda na fedha
za walipa kodi ambazo zingeweza kununua madawa vijijini. Mimi binafsi
sitahudhuria mkutano wa Bunge Maalumu kama makundi hasimu hayatakuwa
yamefikia maridhiano.
Kabwe Zitto, MB/MBMK
No comments:
Post a Comment