JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI JESHI LA POLISI TANZANIA
PRESS RELEASE 22/07/2014 WATU WANANE WAKIWEMO MADAKTARI WASHIKILIWA NA
KUHOJIWA NA JESHI LA POLISI KUTOKANA NA KUTUPWA VIUNGO VYA BINADAMU MAENEO YA
BONDE LA MBWENI MPIJI ENEO LA BUNJU
Kamanda wa polisi kanda Maalumu Dar Es Salaam akielezea tukio hilo mbele ya waandishi wa habari leo jijini Dar Es Salaam.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam
linawashikilia watu wanane na kuwahoji kuhusu tukio la kupatina kwa viungo vya
binadamu vilivyogundulika katika maeneo ya bonde la Mbweni Mpiji ambapo mifuko
ya plastiki ipatayo 85 yenye mabaki ya viungo vya binadamu yaligundulika.
Polisi walipata taarifa 21/07/2014 jioni kutoka kwa wasamaria wema na ndipo
jopo la wapelelezi likiongozwa na Mkuu wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni
ACP. Camilius Wambura walifika hapo majira ya saa 1.00 usiku.
Walipofika katika tukio
waligundua mifuko ipatayo 85 mieusi yenye viungo vya aina mbali mbali vya
binadamu kama vileVichwa,Miguu,Mikono,Mioyo, mapafu, vifua na mifupa ya aina
mbali mbali ya binadamu. Viungo hivyo havikuwa na uvundo au harufu ya aina
yoyote na vilionekana kwamba vimekaushwa na kukakamaa. Katika eneo hilo pia
vilikutwa vifaa vinavyotumika hospitali kama vile mipira ya kuvaa mikononi
(gloves) mifuko miwili iliyotumika ,nguo maalum (apron) zipatazo 20 na karatasi
mbili zenye maswali ya kujibu.
Wananchi wasiopungua 1,000 walifika katika
eneo hilo la tukio lakini hakuna aliyekuwa na taarifa sahihi. Viungo hivyo
vilichukuliwa na kupelekwa hospitali ya Muhimbili kwa uchunguzi zaidi. Aidha
jopo la Wapelelezi chini ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ACP. Japhari Mohamed
walianza uchunguzi mara moja kwa kusaidiana na Daktari wa Jeshi la Polisi
anayehusika na uchunguzi wa miili ya binadamu (Forensic Doctor) ambaye kwa
pamoja walishirikiana na madaktari wengine kutoka hospitali wa Taifa Muhimbili.
Hatimaye uchunguzi wa kina
ulibaini kwamba viungo hivyo kwa mara ya mwisho vilikuwa katika Maabara ya Chuo
Kikuu Madaktari IMTU jijini D’Salaam. Baada ya kugundulika hivyo Polisi wamewakamata
na sasa wanaendelea kuwahoji watu wanane ambao wanasadikiwa kuhusika na miili
hiyo ikiwa ni pamoja na baadhi ya madaktari wa IMTU. IMTU (International Medical
and Technolegical University) ni chuo Kikuu cha Madaktari ambacho pia hufanya
mafunzo ya udakitari kwa vitendo (practical). Jeshi la Polisi Kanda Maalum
litamuhusisha Mkemia Mkuu wa Serikali na hatimaye mara baada ya kukamilika kwa
uchunguzi jalada litapelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua zake
ili sheria ichukue mkondo wake.
S. H. KOVA
KAMISHNA WA POLISI
KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM
No comments:
Post a Comment