Monday, August 18, 2014

HOJA ZA JAJI WARIOBA MATESO BUNGE MAALUMU


Kero za Muungano na taasisi zake zilizotajwa na mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba zimekuwa zikiwatesa wajumbe wa Bunge Maalumu katika mijadala ya rasimu ya Katiba inayoendelea kwenye kamati za chombo hicho.

Miongoni mwa maeneo ambayo yametajwa kusababisha mvutano mkali katika kamati nyingi ni muundo wa Bunge ambao ulitajwa na Jaji Warioba wakati akiwasilisha taarifa ya Tume kuwa una kasoro nyingi ambazo zimesababisha malalamiko kutoka kila upande wa Muungano.

Habari kutoka katika vikao kadhaa vya kamati zinasema baadhi ya wajumbe kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao walikuwa wakiamini katika muundo wa serikali tatu pamoja na baadhi wa Kundi la 201, wamesimama kidete wakitaka yafanyike mabadiliko makubwa ya muundo wa Bunge la Muungano.
“Muundo wanaopendekeza ni kuwa na Bunge la ‘tatu ndani ya moja’ kwa maana kwamba Spika anakuwa mmoja, lakini huku ndani kunatolewa fursa za wabunge wa Tanzania Bara kunapokuwa na masuala yao na wale wa Zanzibar wakutane kwa masuala yao na yale ya muungano basi wote tukutane,” alisema mmoja wa wajumbe wa Kamati Namba Tano.

Ikiwa pendekezo la muundo wa aina hiyo ya Bunge utakubaliwa, majimbo ya Zanzibar yatakuwa na mwakilishi mmoja mmoja, tofauti na sasa ambapo kila jimbo lina mbunge anayeshiriki katika Bunge la Muungano na mwakilishi anayeingia katika Baraza la Wawakilishi.
Watetezi wa muundo huo wanasema pia utajibu kero mbili zilizotajwa na Jaji Warioba ambazo ni wabunge kutoka Zanzibar kushiriki katika mijadala ya mambo yasiyo ya muungano na ile ya sheria zinazopitishwa na Bunge la Muungano kulazimika kupata kibali cha Baraza la Wawakilishi kabla ya kuanza kutumika visiwani humo.

Kwa upande wa wabunge wa CCM wenye msimamo huo, wameujenga katika ahadi waliyopewa na viongozi wao kwamba waunge mkono wazo la kubaki na muundo wa serikali mbili ‘zilizoboreshwa’ hivyo wanataka mabadiliko kadhaa tofauti na wahafidhina ambao wamekuwa wakisimamia muundo wa sasa ubaki kama ulivyo.

“Hawa wakubwa wetu sijui vipi, yaani wanataka kila kitu kibaki kama kilivyokuwa na ikiwa hivyo itakuwa tabu kweli. Ukawa watapata sifa kwamba walichokisema kuwa lengo letu (CCM) ni kubaki na mfumo wa sasa kwa kila kitu itakuwa kweli,” alisema mjumbe mwingine wa Kamati Namba 11.
“Haitakuwa na maana sisi kukaa hapa kwa siku zote halafu tunakuja na yaleyale, lazima hizo serikali mbili zilizoboreshwa zionekane kwa watu, ili watuamini kwamba tulibaki hapa kufanya kazi. La sivyo uamuzi wa kurejea na yaleyale utatuweka pagumu sana hata kwenye uchaguzi ujao wa 2015.”
Kamati ya uongozi

Suala hilo pamoja na mengine kadhaa yaliyowekwa kiporo katika baadhi ya kamati kutokana ugumu wake, yalisababisha Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalumu kukutana kwa siku mbili mfululizo (juzi na jana) kujaribu kuyatafutia ufumbuzi.Juzi kikao hicho kilikutana kwa saa sita, kuanzia saa 5:00 asubuhi na kuahirishwa saa 11:00 jioni, lakini kutokana na kushindwa kumaliza ajenda zake, kilifanyika tena jana kuanzia saa 5:00 asubuhi. Lakini haikuweza kufahamika kuhusu uamuzi wake wa masuala tata yaliyokuwa yakijadiliwa.

Kaimu katibu wa Bunge la Katiba, John Joel juzi alikiri kuwapo kwa kikao hicho lakini hakuwa tayari kueleza kwa undani ajenda zake. Matokeo ya kikao hicho yanaweza kupelekwa kama ‘maelekezo’ ndani ya kamati, lakini huenda yakapata upinzani mkubwa kutoka kwa wajumbe ambao kikanuni wana uwezo wa kuamua kadiri watakavyokubaliana.

Habari zilizolifikia gazeti hili zinasema Ijumaa iliyopita, mjadala katika Kamati Namba 5 uliahirishwa baada ya mjumbe wake, Paul Makonda kusimama kidete akitaka muundo wa Bunge ufanyiwe marekebisho tofauti na ulivyo sasa, hoja ambayo iliungwa mkono na wajumbe wengine kadhaa.

Habari zinasema suala hilo lilisababisha mvutano mkali kutokana na wajumbe wa Zanzibar kuipinga hasa pale inapoonekana kwamba nafasi zao za uwakilishi zitapungua kutoka mbili za sasa kwenye majimbo hadi moja.
“Baadhi yao wanajenga hoja kwamba eti suala hilo litahatarisha Muungano na sisi tumewaambia yanapokuja mambo ya kwao wanakubali, lakini likija la upande wa Bara wanaleta sababu. Sisi hatutakubali katika hili,” alisema mjumbe mwingine wa kamati hiyo.

Mwenyekiti wa Kamati Namba 5, Hamad Rashid Mohamed alisema mjadala kuhusu suala hilo ni wa kawaida na kwamba leo watalifanyia uamuzi wa mwisho kwa maana ya kupiga kura ya mapendekezo.
Hoja nyingine ambayo iliibuliwa na Tume ya Warioba na ambayo imekuwa ikisumbua vichwa vya wajumbe katika kamati ni nafasi ya Makamu wa Rais ambayo imekuwa na mapendekezo ya kuwapo kwa nafasi tatu lakini baadhi yao wakipinga wazo hilo. Jaji Warioba alisema wananchi wa Zanzibar walilalamika kwamba Rais wao hana nafasi ya kutambuliwa katika Muungano hivyo walitaka arejeshwe katika nafasi ya makamu wa Rais.

Hata hivyo, hofu ambayo imeonekana miongoni mwa wajumbe hasa wanachama wa CCM ni iwapo rais atatoka nje ya chama chao, hivyo kupendekeza kwamba wawepo makamu watatu, hoja ambayo pia inapingwa. Hoja hizo zinatarajiwa kushika mjadala wakati kamati nyingine zitakapoendelea na vikao.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...