Nikiwa kama CEO wa Bhitz Music Group na Producer ambaye napigana kama
producers wengine kuusogeza muziki wa Tanzania katika level fulani,
sikupendezwa kabisa na jinsi ambavyo baadhi ya watu walivyoizungumzia
Bhitz na jinsi ambavyo baadhi yao wanaichukulia.
Kutokana na yote yaliyozungumzwa na baadhi ya wasanii ambao
tulitofautiana nao kikazi, wengi wametuchukulia kama sisi ni wagomvi na
wanyonyaji.
Lakini ukweli ni kwamba hakuna msanii ambaye alishatengeneza faida ya
kifedha kwa Bhitz na wasanii hao walikuwa wakifanya kazi bila malipo
yoyote na hata walipokuwa wakifanya shows tulikuwa tukiwaachia pesa kwa
kuwa tulifahamu bado muda mzuri wa mavuno kulingana na ubinadamu,
makubaliano na malengo, hivyo hakuna ukweli kuhusu hilo.
Hata hivyo, tumeyachulia yote yaliyotokea kama sehemu ya changamoto
katika kazi hii ngumu ya muziki Tanzania ambayo kwa kiasi kikubwa
watayarishaji wa muziki hawafaidiki nayo kama ilivyo kwa wasanii ambao
wamejaliwa kuwa na ushawishi mkubwa zaidi kwa jamii na kuaminika mara
moja kwa kile wanachokisema kuhusu sisi pale tunapotofautiana.
Kwa bahati mbaya, mipango tunayopanga nao tunapokuwa studio ama
makubalinao mengi tunayoweka kwa ajili ya kazi zao hayajulikani kwa
umma, na pindi wanapoyakiuka na kusababisha sisi kurudi nyuma
tunaonekana wakosaji na wacheleweshaji wa maendeleo yao.
Naamini wasanii na sisi ndio tunaofahamu ukweli ni upi kati ya yote
yaliyosemwa kupitia media kwa kuwa tunafahamu wapi tumetoka pamoja,
tulikubaliana nini na wapi tulipotofautiana na nani aliacha reli ya
makubaliano.
It’s a new chapter, na tunawatakia kila la kheri
wasanii wote waliopita Bhitz na milango iko wazi kwa msanii yeyote wa
Tanzania. Lengo letu ni kuendelea kuisapport jamii yenye vipaji kwa
maendeleo ya taifa hili linalosifika kwa vipaji.
Nafasi ipo PI kwa wasanii wote walioondoka na kuacha kazi zao Bhitz,
najua wanajua ni muziki mzuri na tusingependa kuona ukipotea au tukiotoa
kwa kufuata ratiba tulizowekeana awali wakati ambapo wao hawapo.
Wasanii wanaweza kufuata nyimbo hizo na tutakuwa na makubaliano fair
ili maisha ya muziki tulioutengeneza kwa ubunifu wa hali ya juu
yaendelee na watanzania wafaidike kwa kuusikiliza.
Tunaamini uwezo wa Bhitz kuinua vipaji ambavyo havina majina makubwa
na kuvifanya ‘brand’ ni baraka ambayo inabidi iendelee kwa vipaji
vingine ambavyo bado havijajulikana na vina uwezo mkubwa.
Hivyo, tunapenda kuuarifu umma wa watanzania kuwa Bhitz imefungua
ukurasa mpya na hatuendelei kuyashikilia tena matatizo yaliyokuwepo na
wasanii hao.
Tunafurahi pia kuona muziki tuliotengeneza nao wakati tukiwa pamoja
unawapa nafasi kubwa na kuwasogeza katika ngazi nyingine, tunaamini
wanatoa shukurani zao kwa Mungu na zinatufikia kwa kiasi tunachostahili.
Tunaamini tutafika mbali na tumekomazwa zaidi na yaliyojiri kwa kuwa tumejifunza pia, yale ni mapito.
Music shall continue to live and flow in our bloods, we
shall support Tanzanian music and musicians with all our hearts, We
shall not give up because we are a part of this beautiful musical
community in Tanzania.
Katika hatua nyingine, ningependa kuungana na producers wengine
kuyatoa ya moyoni pia kuhusu kilio cha watayarishaji wa muziki Tanzania
ambacho kimeendelea kuonekana kama kilio cha samaki huenda ni kutokana
na idadi yetu ndogo kulinganisha na wasanii au mfumo mzima wa Industry
ya Tanzania ulivyo mbaya na umezoeleka.
Producers wengi Tanzania tumekuwa tukitumiwa na baadhi ya wasanii
kama daraja la mafanikio yao na kisha kutupata matope au kuuambia umma
kuwa sisi ndio tumewakosea sana na tunawanyonya.
Laiti kama wasanii hao wangekuwa wanaeleza angalau mazuri
wanayofanyiwa na producers. Kwa bahati mbaya sifa wanazotumwagia
tunapokuwa studio tunafanya kazi huishia studio na umma husikia tu wimbo
mzuri ukiwa umetoka. Sifa zetu tunazopewa zimekuwa ‘perishable’ ingawa
kazi tunayofanya huishi miaka yote na hutumiwa na msanii husika.
*Kwa mazoea ya soko la Tanzania, producers wengi huwa na moyo wa
mshumaa na hata kuwatengenezea wasanii wetu midundo au nyimbo bure.
Lakini wapo pia ambao huwalipisha wasanii kiasi cha fedha ambacho kwa
uhalisia wa kazi na matunda ya kazi hii sio halali/sio fair bali ni bei
zilizozoeleka tu.
Kwa uhalali wa ‘intellectual works’ wahusika wakuu huvuna matunda
pamoja kwa kugawana asilimia kila wakati ambapo kazi hiyo itakapokuwa
ikiingiza pesa. Lakini kwa Tanzania ni kama producer humuuzia haki
miliki ya kazi nzima msanii kwa shilingi kadhaa au hata bure na kisha
msanii kuingiza mamilioni kwa miaka mingi kwa kuuza au ku-perform kazi
ile.
Hata kama kweli tasnia ya sanaa ya muziki kwa Tanzania bado
inawanyonya wadau kwa ujumla, kati ya hao wanaonyonywa tumkumbuke
producer ambaye yeye ananyonywa hadi damu ya mwisho na kisha kuchafuliwa
pale anaponyoosha mikono yote kutaka mambo yaende sawa.
Hebu fikiria, kama kweli mgao wa matunda ya kazi yangekuwa sawa kwa
asilimia kadhaa kwa kila kazi ambayo producer amefanya, producer kama
P-Funk Majani angekuwa na maendeleo kiasi gani kutoka kwenye muziki
pekee? Sisemi moja kwa moja kama aliofanya nao kazi walimnyonya,
inawezekana alinyonywa na mfumo ulivyo.
Lakini ni wasanii wangapi tumeshawasikia wakitaja mafanikio makubwa
waliyoyapata kwenye muziki kwa hits chache au hata hit moja tu. Je,
umeshajiuliza producer wake alipata nini?
Je, ni producers wangapi ambao wametengeneza hits kibao
zilizowapeleka wasanii mbali sana lakini wao wamebaki na hali ngumu
kimaisha huku wakiendelea kunyonga midundo na kuambuliwa sifa za studio?
Uzalendo na moyo wa pekee tuliopewa usiokata tamaa kwenye
muziki huu ndicho kitu pekee kinachotufanya tuendelee kuwekeza kwenye
huu muziki na kuinua vipaji vipya na kuendeleza vilivyopo kwa imani kuwa
ipo siku tutavuna matunda.
Lakini kwa nini hiyo siku isiwe LEO? Itawezekana kama tutaungana na kuungwa mkono na wapenzi wa muziki mzuri.
Nisingependa kutaja majina ya producers wanaowalilia wasanii lakini
karibia producers wote wamekuwa wakifanya hivyo na vilio vyao hupuuzwa
tofauti na vilio vya wasanii.
Ndugu yangu Master Jay yeye amewahi hata kutoa kauli nzito kuwa
wasanii ni wezi wanatuibia na wanatunyonya sisi maproducer. Alikazia
kuwa wizi huu wa wasanii ni wa aina yake kwa kuwa huiba nguvu ya
producers na kisha kujitangaza kuwa wameingiza kiasi kikubwa cha fedha
kwa kazi ile ile.
Lamar amewahi kusema wasanii wanapokuja studio huwa wapole na
kukubaliana mengi kuhusu wimbo lakini wimbo unapotoka na wao kufanikiwa
huwasahau kabisa producers walioumiza nao kichwa mwanzoni na hata
‘kuwavimbia’. Lamar pia aliwahi kupata matatizo ya kimkataba na msanii
wa Tanzania ambaye aliamua kusaini tena na Candy and Candy ya Kenya ili
hali akiwa na mkataba mwingine na mambo yaliisha kimya kimya.
Producer Dupy yeye aliweka wazi kuwa sisi producers wa Tanzania ni
masikini kulinganisha na wasanii ambao tunafanya nao kazi na kueleza
ukweli kuwa hata wale wanaoonekana maisha yao ni mazuri ni wale ambao
wanaingiza kipato kupitia shughuli nyingine tofauti na muziki.
Mimi pia ni mmoja kati ya producers ambao wanapata fedha kupitia
shughuli nyingine na fedha hizo naziwekeza tena kwenye muziki kwa imani
kuwa ipo siku mambo yatakuwa mazuri lakini mara nyingi wasanii unaopanga
nao studio wanapopata mabawa (mafanikio) huruka na kueleza mabaya na
sio mazuri mliyofanya nao yaliyowapa hayo mabawa.
Sisemi kuwa sisi hatuwakosei wasanii, tunawakoseana kwa kuwa sisi pia
ni binadamu japo sio kwa kiasi hicho wanachosema. Kukoseana katika kazi
ni jambo la kawaida. Kukwaruzana wakati wa ujenzi ni kawaida pia.
Lakini kwa kuwa msanii huyo tayari ni brand, hasara kubwa huwa kwa
producer ambaye inabidi aendelee kufanya kazi nyingine na watu wengine
kwa kuanzisha upya malengo yake huku akiwa amemfaidisha tayari msanii
huyo (Tayari ni brand).
Nyimbo tunazotengeneza nyingi studio tukisubiri msimu wa ‘mvua’
tuupush zinapobaki huwa hasara kwa producer kwani wao wanaweza kwenda
kwa mwingine na wakazirudia. Je, producer anapata faida gani kwa kazi
aliyoifanya tayari?
*Imefika wakati ambapo producer inabidi aheshimiwe kwa sababu bila
yeye kusingekuwa na wasanii wengi wanaotamba hivi sasa. Hii itaongeza
nguvu pia ya kazi kwa producers wapya nchini.
Producer alipwe vizuri kwa sababu anapomlipwa vizuri na yeye ubunifu
na utendaji wake wa kazi unakua kwa kiwango kikubwa. Pia atapata uwezo
wa kununua vitendea kazi bora zaidi vitakavyomsaidia kuingiza muziki
wetu kwenye ushindani wa soko la muziki Afrika na duniani kwa ujumla.
Naamini ipo siku hata haki za producer katika muziki alioutengeneza
Tanzania zitazingatiwa ikiwa ni pamoja na kuvuna asilimia fulani ya
muziki wake pale unapotumika kwenye miito ya simu, na biashara nyingine.
This is the time, sisi tunaendelea na kazi na tunawakaribisha wasanii wote.
Hermes B. Joachim
No comments:
Post a Comment