Wajumbe wa Kamati Namba 10 ya Bunge Maalumu, juzi walijikuta
katika wakati mgumu baada ya kubanwa kwa karibu saa nzima na Mbunge wa Mpanda
Mjini (Chadema), Saidi Arfi. Habari kutoka ndani ya kamati hiyo zinasema tofauti na fikra
za wajumbe wengi kwamba mjumbe huyo angewaunga mkono kwa kila jambo, hali
imekuwa tofauti kwani amekuwa na misimamo kama iliyoonyeshwa na wajumbe wa Ukawa
ambao wamesusia Bunge hilo.“Yule bwana pamoja na mjumbe mmoja hivi kutoka kundi la 201
upande wa Zanzibar wametuhenyesha sana maana misimamo yao ni ileile ya Ukawa,
yaani wameamua kuandika maoni ya wachache, jambo ambalo awali hatukulitarajia,”
alisema mmoja wa wajumbe.
Chanzo cha habari kimebaini kuwa mbunge huyo kutoka Zanzibar ni
Adil Mohamed Ali ambaye pamoja na Arfi wameamua kuandika maoni ya wachache
kuhusu eneo la madaraka ya Rais lililokuwa likibishaniwa.
Kanuni ya 32 (10) inatoa fursa kwa wajumbe wasiokubaliana na
uamuzi kwenye kamati kuandika maoni ya wachache na maoni hayo yamepewa dakika
60 (saa moja) kusomwa bungeni kwa mujibu wa Kanuni ya 33 (5).
Juzi, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo namba 10, Salim
Awadhi Salim akizungumza na waandishi wa habari alisema walilazimika kuweka
kando ibara za 72 na 73 ambazo zinazungumzia mamlaka ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano baada ya kutokea mvutano makali.
“Sura namba saba ibara ya 72 na 73 ambayo inahusiana na
uongozi tuliahirisha ili wajumbe waweze kutafakari,” alisema Salim huku
akifafanua kwamba wajumbe wengi walisema kuwa majukumu aliyopewa Rais katika
Katiba ya sasa ni mengi, hivyo apunguziwe.
Habari kutoka ndani ya kamati hiyo zimesema mbali na
madaraka ya Rais, suala jingine lililozua mvutano likimhusisha Arfi na Ali ni
pendekezo la wajumbe wa kamati hiyo kutaka uwapo wa makamu watatu wa rais.
“Kulikuwa na pendekezo kwamba tuwe na makamu wa rais watatu
ambao ni yule anayetokana na mgombea mwenza, Rais za Zanzibar ambaye anakuwa
makamu wa pili na makamu watatu anakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania,” kilisema chanzo chetu.
Habari zinasema kutokana na hali hiyo, Arfi na Ali waliibua
hoja kwamba ikiwa kuna pendekezo la makamu watatu wa rais, kwa nini pendekezo
la serikali tatu linakataliwa na hapo ndipo mvutano ulipoanzia na kusababisha
mjadala mkali uliochukua takriban saa nzima.
Alipoulizwa jana, Arfi hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo
kwa maelezo kwamba kama kuna chochote kitakachotakiwa kufahamika basi
kitawasilishwa bungeni baada ya kamati kumaliza kazi yake.
“Mimi sidhani kama ni busara kuzungumza kwa sasa, kuweni na
subira maana mahali sahihi pa kusemea mambo haya ni kule bungeni,” alisema Arfi
ambaye ameingia katika mgogoro mkubwa na chama chake kutokana na kukiuka
makubaliano ya kususia vikao hivyo.
Kwa upande wake, Ali hakuthibitisha wala kukanusha kuwapo
kwa mpango wa kuwasilisha maoni ya wachache, lakini akasema asingeweza
kuzungumza kwani alikuwa na kazi nyingi ndani ya kamati.
Habari kutoka ndani ya kamati hiyo pia zilisema kuwa wajumbe
hao wawili wamekuwa wakivutana na wenzao pale kunapotolewa mapendekezo ya
kufutwa kwa maneno ‘shirikisho’ au ‘Tanganyika’.
“Hoja yao ni kwamba kwa nini tufute maneno hayo wakati Bunge
Maalumu halijaamua kuhusu muundo wa muungano?Tumekuwa kwenye wakati mgumu kweli na katika baadhi ya ibara
tumeacha hivyo,” kilifafanua chanzo chetu.
No comments:
Post a Comment