Dodoma. Wenyeviti wa vyama vya Upinzani vya Chadema, Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha NCCR-Mageuzi, jana usiku walikutana ili kutoa kauli ya pamoja, kutokana na hotuba ya ufunguzi wa Bunge kwa maelezo kuwa tayari Rais amevuruga mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya.
Wakati viongozi hao wakikutana, Mwenyekiti wa
Chama cha DP Mchungaji, Christopher Mtikila alisema, Rais ameingilia
mchakato na kutoa maelezo jinsi ya kuandika Katiba.
Wakizungumza na gazeti hili jana mara baada ya
hotuba hiyo, Freeman Mbowe, James Mbatia na Profesa Ibrahim Lipumba,
walisema wameipokea kwa masikitiko makubwa hotuba hiyo.
“Tunakwenda kujadili hotuba ya Rais na tutatoa msimamo wetu,” alisema Mbowe.
Awali Katibu wa muda wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), Julius Mtatiro alisema Rais Jakaya Kikwete amevuruga
mchakato wa Katiba, kwani walitarajia angetumia mamlaka yake kama Rais
kuwaunganisha.
“Rais tulitarajia angeongea kama mkuu wa nchi,
lakini amezungumza kama Mwenyekiti wa CCM na kutoa msimamo juu ya muundo
wa Muungano jambo ambalo hatukulitegemea,” alisema Mtatiro.
Alisema kwa Rais kutoa msimamo ni sawa na mwongozo jambo ambalo limevuruga mchakato mzima.
Hofu ya kuvunjika Bunge
Wakizungumza nje ya Bunge, baadhi ya wajumbe
wameeleza kuwa hotuba ya Rais Kikwete kama ikitekelezwa uwezekano wa
kupata Katiba Mpya utakuwa mgumu.
Mjumbe Luhaga Mpina alisema kwa jinsi rasimu
ilivyoandikiwa na kama muundo wa serikali mbili ukipita basi rasimu ya
Katiba itabidi iandikwe upya.
“Rasimu yote imetengenezwa kwa mfumo wa serikali tatu sasa hapa kuna hatari ya Bunge kukwama ,” alisema.
Mtatiro kwa upande wake alisema sasa kuna hofu ya
kushindwa kupatikana Katiba Mpya kwani Rais amewachanganya wajumbe na
kama watapitisha maoni yake itabidi rasimu kuandikwa upya.
Mjumbe Mustapha Akoonay, alisema upatikanaji wa katiba upo shakani kwani sasa upinzani utakuwa mkubwa juu ya muundo wa muungano.
“Kwa sasa nadhani itabidi turudi upya kwa wananchi kupata kura ya maoni juu ya muundo wa muungano,” alisema.
Lucy Owenya alisema Rais amegeuza mkutano wa
Bunge kuwa ni mkutano wa Chama Cha Mapinduzi, kwani ameshindwa kabisa
kutoa mwelekeo wa nchi na badala yake ametoa msimamo wa CCM.
“Kutokana na hili, naamini kabisa Bunge
halitakuwapo na ni bora iwe hivyo kwa kuwa amejibu hotuba ya Warioba na
kwa maana hiyo amepingana na mawazo ya wananchi.”
Godbles Lema alisema kuwa Rais hakuja kuhutubia taifa bali alikuja kufanya semina na kujibu hotuba ya Warioba.
Mjumbe huyo ambaye ni mbunge wa Arusha Mjini
alionyesha shaka kuwa baada ya muda wa wiki tatu hakutakuwa na Bunge la
Katiba kwa kuwa wako baadhi ya watu ambao hawatakubali kilichofanywa na
Rais Kikwete.
“Waliochukua fedha ni vyema wakaenda kumalizia
nyumba zao kwa kuwa kiongozi wetu amefanikiwa kwa kiasi kikubwa
kuwafurahisha wanaCCM lakini kwa Watanzania hatutakubali,” alisema Lema.
John Cheyo alisema, “Mimi ninachokiona ni
maridhiano tu, suala la kufumua rasimu halinipi shida kwa kuwa vitu
vyote vinavyoletwa bungeni huwa ni mali ya Bunge na hivyo tutafanya
tunavyoona sisi inafaa.”
Mchungaji Peter Msigwa, alisema kuwa kosa kubwa
ambalo lilifanywa na upinzani ni kukubali na kuruhusu Jaji Warioba
atangulie kuwasilisha rasimu yake akasema hilo ndilo lililowagharimu.
Alitaka Bunge livunjwe mara moja ili warudi kwa
wananchi wakaamue na kuwahukumu kutokana na kile ambacho walikifanya
katika Bunge ambalo kwa maoni yake wamekula fedha za walipa kodi bure.
Naye Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa aliipongeza hutuba ya Rais Jakaya Kikwete ya uzinduzi wa Bunge la Katiba.
Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge la Katiba,
alisema kwa kifupi hotuba ya Rais Kikwete ni nzuri. Lowassa alitoa kauli
hiyo, wakati akitoka nje ya Bunge, muda mfupi baada ya Rais Jakaya
Kikwete kumaliza hotuba ya uzinduzi wa Bunge hilo.
Naye Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Mchungaji Ernest Kadiva, alisema hotuba ya Rais imetoa mwanga kwa wajumbe.
“Rais ameonyesha upungufu wa hoja mbalimbali hasa
katika mfumo wa serikali tatu na sasa ameacha kazi ya kuamua tuwe na
mfumo wa serikali mbili au tatu ni ya wajumbe,” alisema Mchungaji
Kadiva.
Hata hivyo, mjumbe mmoja ambaye hakupenda kutaja
jina lake alisema Rais alizungumza kama si mkuu wa nchi bali Mwenyekiti
wa CCM kwa sababu amesimamia hoja za chama chake.
Alisema hata kama mapendekezo ya Rais Kikwete
yatatekelezwa, kamwe hayatakuwa mwarobaini wa muungano. Mbunge wa
Mwibara, Khangi Lugora alisema hotuba hiyo waliitarajia na ndio maana
kulikuwa na ubishi wa nani atangulie kati ya Jaji Joseph Warioba na yeye
kwa mujibu wa kanuni.
“Hotuba ilikuwa ikijaribu kumjibu Jaji Warioba na
kwangu mimi nilikuwa naona kuwa Rais naye alikuwa anachangia katika
kuitunga Katiba kwa kupitia hotuba yake hiyo. Tumeyasikia na sisi
tutakwenda kutafakari katika kutunga Katiba ambayo itakuwa ya Watanzania
wote,” alisema.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema)
Mkiwa Kimwanga, alisema kilichofanyika ni Rais kwenda kutoa uamuzi juu
ya mchakato uliokuwa ufanywe na Bunge hilo.
Kwa upande wake, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema
hakuitendea haki Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwamba Bunge hilo
haliwezi kutengeneza Katiba ambayo inalenga katika mfumo wa serikali la
mbili.
“Itakuwa ni vigumu zaidi kupata Katiba Mpya,
alikuwa anapinga mambo ya msingi yaliyoelezwa katika rasimu ya kwanza.
Hayo angeyaeleza katika hatua ya awali ili rasimu hiyo ibadilishwe na si
katika hatua hii ya mwisho kabla ya kwenda kupigiwa kura na wananchi,”
alisema.
Alisema ndani ya siku 70 haiwezekani kubadili
rasimu hiyo ambayo imejikita katika muundo wa serikali tatu kwenda
katika muundo wa serikali mbili.
Ezekiah Olouch alitahadharisha wajumbe wenzake kutodharau maoni ya wananchi waliyoyatoa katika rasimu hiyo ya pili.
Alisema haiwezekani tume zote ambazo zimeundwa
kuangalia aina ya muundo wa serikali zije na jibu moja kuwa namna ya
kuimarisha muungano ni kuwapo kwa serikali tatu.
Jussa Ismail Ladu alisema kwa ufupi kwamba hotuba ya Rais Kikwete imekuwa yenye sura ya CCM zaidi.
Naye Mbunge wa Lulindi, Jerome Bwanausi, aliielezea hotuba ya
Rais kuwa imeibua mambo mengi ambayo baadhi ya watu walikuwa wakiyaelewa
tofauti, hivyo imeweka uelewa mzuri katika baadhi ya maeneo.
Profesa Costa Mahalu alisema ni hotuba ambayo
imewaachia changamoto, hasa katika eneo la muungano kwa sababu
wanahitajika kuunda muungano usiotetereka.
Credit kwa Mwananchi CL
Credit kwa Mwananchi CL
No comments:
Post a Comment